Rais Dkt.Samia aridhia tena kutoa msamaha hadi Aprili 30

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameridhia kwa mara nyingine tena kutoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi, ambapo wananchi walio na malimbikizo amewapa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo kuanzia sasa hadi Aprili 30, mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo Februari 14, 2023 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Wadau wa Sekta ya Ardhi nchini katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

"Naomba nichukue fursa hii kuwajulisha kuwa Mheshimiwa Rais ameridhia kwa mara nyingine tena,baada ya kuombwa na kuridhia, kuongeza kipindi cha msamaha hadi mwezi Aprili, 2023,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Amefafanua kuwa,uamuzi huo umefikiwa kutokana maombi mengi yaliyowasilishwa na wananchi, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt.Samia akaendelea kutumia hekima na busara zake kuongeza muda tena.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema kuwa, hayo ni matokeo ya mkutano wa kwanza walioufanya Mei 23, 2022 ambapo katika mkutano huo wadau hao walipata fursa ya kutoa maoni, hoja na mapendekezo ya kuboresha utoaji huduma katika Sekta ya Ardhi.

Amesema, kupitia mkutano huo wa awali, wizara imeyafanyia kazi maoni na hoja za wachangiaji 53 kwenye maeneo makubwa 15.

Kufuatia hoja na maoni hayo, Waziri Dkt.Mabula amesema, wizara imeandaa Bangokitita linalotoa ufafanuzi wa kina kuhusu walivyoshughulikia maoni, hoja na mapendekezo yaliyotolewa.

"Naomba nitoe mrejesho kwa ufupi wa baadhi ya maoni, hoja na mapendekezo muhimu yaliyofanyiwa kazi hadi sasa, kwanza, madeni na malimbikizo makubwa ya kodi ya pango la ardhi kwa wamiliki wa vipande vya ardhi nchini.

"Hoja ya malimbikizo makubwa ya kodi imefanyiwa kazi ambapo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi, ambapo wananchi walio na malimbikizo walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo kuanzia Julai hadi Disemba,2022,"amefafanua.

Pia amebainisha kuwa,katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Januari 2022, wizara ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 99.9 sawa na asilimia 70.8 ya lengo la makusanyo ya shilingi Bilioni 141 kwa miezi saba.

"Makusanyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 yameongezeka kwa shilingi bilioni 33.9 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2021/22 uliopita.

"Wananchi 6,211 wamenufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo shilingi 11,931,537,409.80. Serikali inaamini kuwa fedha hizo zilizosamehewa zimeleta nafuu kwa wahusika na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.

"Nitumie fursa hii kumshukuru Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kusamehe kiasi kikubwa hicho kwa lengo la kuwaondolea mzigo wa madeni wananchi na taasisi mbalimbali,"amebainisha Waziri Dkt.Mabula.

Amesema, pamoja na mafaniko yaliyopatikana katika utekelezaji wa hoja hii, zipo changamoto mbalimbali zilijitokeza zikiwemo kushindwa kukamilika kwa baadhi ya miamala ya wananchi waliokuwa tayari kulipa deni la msingi.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, ni changamoto ya mtandao iliyosababishwa na wamiliki wengi kutumia njia za ki-eletroniki kulipa kodi kwa wakati mmoja.

“Hivyo, ninatoa rai kwa taasisi, mashirika ya umma na wananchi wote kutumia muda uliotolewa na Mheshimiwa Rais hadi Aprili 30, 2023 kunufaika na msamaha wa riba uliotolewa na Serikali kulipa deni la msingi (principle amount) ili wasamehewe riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi,”amesisitiza Waziri Dkt.Mabula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news