Rais Dkt.Samia atafakari kuhusu kuongeza wizara mpya, atoa onyo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, anatarajia kuunda wizara nyingine mpya ambazo zitakuwa chini ya Ofisi ya Rais, akieleza kuwa zitahusiana na Msajili wa Hazina, Tume ya Mipango na Uwekezaji.

“Tumeona watu wanauliza, kuna Katibu Mkuu wa Uwekezaji, mbona hana Waziri. Tumemtambulisha Katibu Mkuu atusaidie kupanga tunachotaka.

Tunataka maeneo matatu muhimu yarudi chini ya Ofisi ya Rais. Tukimaliza mchakato wa kutunga sheria zitakuwa wizara kamili… lakini kwa sasa tunaleta Msajili wa Hazina, Tume ya Mipango na Uwekezaji-TIC;

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Februari 27, 2023 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Februari 26, 2023.

Pia alisema kuwa, "Nilidhani kuwa lile jeshi (Baraza la Mawaziri) lililopo tungekwenda nalo mpaka tuvuke ule mwamba wa kuingia upande wa pili, katika safari ajali zinatokea mwingine anajikwaa anaanguka,"ameeleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Wakati huo huo, amemtaka Mheshimiwa Abdalah Ulega aliyechukua nafasi ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuhakikisha ugomvi wake na wao utamalizwa kwa kufanya kazi na anataka kuona Mifugo na Uvuvi inanyanyuka.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Abdallah Hamis Ulega kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 27 Februari, 2023.

"Nakuamini na nadhani utaweza, kama wakati ule ulikuwa hufanyi, kwa sababu ulikuwa chini ya mtu sasa utaonekana unafanya kwa sababu hauko chini ya mtu au na wewe utakuwa kama wale, safari bado ni ndefu tuna miaka miwili mbele yetu, nikuombe ukafanye kazi.

"Tumejitahidi kunyofoa katika maeneo mliyopo kujaza nafasi hizo, tukijua kuwa kila mtu anaelewa eneo lake alilopo," amesema Rais Dkt.Samia.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema mabadiliko hayo pia yamevuta watu walio nje ya Serikali kwa lengo kuwa watakuja na mawazo mapya na kuona ndani ya Serikali nini kinafanyika wakichanganya na wao mambo yatakwenda vizuri.

"Tutaendelea kunyofoa huko na kuleta ndani ili atusaidie Serikali kwa sababu akikaa nje kazi ni kulaumu tu, hajui ugumu uliomo ndani ya Serikali, wakiingia tutafanya nao watupe uzoefu wao waone yaliyopo serikalini ili twende kwa pamoja.
 
“Ngoja niweke wazi. Hii itakuwa mara yangu ya mwisho kufanya mabadiliko madogo kwa sababu ya kutoelewana miongoni mwa viongozi katika wizara hiyo hiyo. Sitavumilia hili na pale ambapo kutakuwa na mkanganyiko nitalazimika kuwashusha nyote …namaanisha Waziri, Naibu na Makatibu Wakuu,”ameongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news