Rais Dkt.Samia azidisha tabasamu kwa vikundi vya wanawake,vijana na wenye ulemavu Ushetu, Mheshimiwa Cherehani atoa neno

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa mkopo wa shilingi milioni 361,100,000 kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati akikabidhi hundi katika hafla iliyofanyika wilayani Ushetu tarehe 4 Februari 2023, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Peter Cherehani amesema kuwa fedha hizo ni maelekezo ya serikali kwa Halmashauri zote nchini kutoa asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya makundi hayo muhimu.
Dkt. Cherehani amewataka wanufaika hao wa mkopo kuhakikisha kuwa wanatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujikwamua na wimbi la umasikini na si vinginevyo.

Amewasihi wanufaika hao kutumia vizuri mikopo hiyo na kuhakikisha kuwa miradi waliyokusudia kutekeleza wanaifanyia kazi ipasavyo ili waweze kurejesha mikopo kwa ajili ya kukopeshwa watu wengine.

“Pelekeni fedha kwenye eneo lililokusudiwa, ninajua wakati mwingine mnapata ushawishi kutoka kwa watu wengine lakini fedha hizi sio za kwenda kuhonga, kafanyeni maendeleo yenu na familia zenu,”amesisitiza Dkt.Chereheni.
Amesema kuwa, fedha hizo hazipaswi kuwa sehemu ya mtafaruku katika familia badala yake ziwe sehemu ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya familia.

Pamoja na kukabidhi fedha hizo kwa wanufaika hao pia, Mheshimiwa Cherehani amekabidhi pikipiki kwa vijana kwa ajili ya kufanya biashara ya bodaboda itakayowaingizia kipato.

Amewasihi wanufaika hao kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii ili kuweza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi 17 kati ya vikundi 70 vilivyoomba mikopo ambapo vikundi 11 ni vya wanawake, vikundi vitano ni vya vijana huku kikundi kimoja kikiwa cha watu wenye ulemavu.
Nao wanufaika wa mikopo hiyo ambao ni wakazi wa Ushetu wamempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mikopo hiyo kupitia Halmashauri za Wilaya huku wakisema kuwa watafanya kazi kwa bidii ili kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news