NA FRESHA KINASA
MKUU wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amewataka Wakuu wa wilaya zote mkoani humo kuwajibika kikamikifu kufanikisha lengo la Serikali katika maeneo yao kwa ufanisi la utoaji wa chakula kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni kwa asilimia 100.
Pia, ameagiza utaratibu wa kuuza vitu mbalimbali shuleni unaofanywa na watu ikiwemo barafu usiendelee tena katika shule za Mkoa wa Mara badala yake ameagiza Maafisa Elimu kusimamia kila shule kwa kuhakikisha inaanzisha duka ili kuuza vitu muhimu ambavyo vitawasaidia wanafunzi kupata mahitaji muhimu.
Sambamba na kusimamia kila shule iweke utaratibu wa kupika uji shuleni kwa ajili ya wanafunzi kusoma kwa ufanisi.
Ameyasema hayo leo Februari 6, 2023 wakati akizungumza katika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa afua za lishe ngazi ya mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Mjini Musoma.
Amesema, programu ya watoto kula shule ni takwa la serikali ambalo viongozi hao katika maeneo hayo wanawajibu wa kulisimamia kikamilifu kwani bado utekelezaji wake haujafanikiwa kama inavyotakiwa. Ambapo mkoa huo kwa mwaka jana ulikuwa wa mwisho hivyo wawajibike kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.
Amesisitiza viongozi wote mkoani Mara kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi kuwatumikia Wananchi pamoja na kuleta mabadiliko kwa Wananchi ambao bado wanakumbatia mila na desturi zinazosababisha watoto wasile chakula shuleni.
Kwa upande wake Dkt. Zabron Masatu Katibu Tawala msaidizi upande wa Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii mkoani humo amesema kuwa suala la lishe kwa wanafunzi wakiwa shuleni ni muhimu kutekelezwa kwa ufanisi kwani lina faida kubwa kwa afya ya wanafunzi katika kuwezesha wasome kwa ufanisi.
Naye Benson Sanga, Afisa Lishe Mkoa wa Mara amesema kuwa, lengo la Programu hiyo ni kuhakikisha wanafunzi wanakula wakiwa shuleni na sio utaratibu uliopo katika baadhi ya shule wanafunzi kupewa muda kwenda nyumbani kula.
"Lengo ni wanafunzi kula chakula wakiwa shuleni pale pale sio kwamba wanapewa muda kwenda kula nyumbani. Kwa hoyo kinachotakiwa ni kila shule kuweka utaratibu wa kuwapa chakula wanafunzi wakiwa shuleni hapo,"amesema Benson Sanga.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vincent Naano amesema kuwa amejipanga vyema kuhakikisha anafanikisha suala hilo kwa ufanisi katika Wilaya ya Bunda kwa kuweka mpango shirikishi na kushirikiana na Halmashauri za Wilaya hiyo kuweka Sheria ndogo ndogo zitakazosaidia kutekelezwa kwa ufanisi.
Benedict Raymond Mangulu,Mkuu wa Idara ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Rorya amesema kuwa, faida za wanafunzi kula chakula wawapo shuleni inafaida kubwa sana katika kutatua tatizo la utoro kwa wanafunzi.
"Mwaka Jana tulipokaa kikao Serengeti tulibaini tatizo la utoro wa wanafunzi kwa asilimia 26 kwa mkoa wetu wa Mara. Sasa faida za Watoto kula shuleni ni pamoja na kuongeza usikivu, kubooresha afya ya akili kwa Watoto, kuimarisha mahudhurio shuleni pamoja na kuondoa utoro shuleni kwa hiyo Jambo hili linafaida kubwa sana,"amesema Benedict Raymond.