NA FRESHA KINASA
MKUU wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amezindua mfumo wa Mobile -Mama (M-mama) katika Mkoa huo unalenga kupunguza vifo vya wajawazito wanaojifungua na watoto katika kuhakikisha dhamira ya Serikali inazidi kufanikiwa ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya, waganga wakuu wa halmashauri, wenyeviti wa halmashauri katika kikao cha uzinduzi wa mfumo huo kilichofanyika Februari 13, 2023 katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya mkuu wa Mkoa huo Mjini Musoma. Meja Jenerali Mzee amewataka Wakuu wa Wilaya na Viongozi wote kujipanga vyema kuutekeleza mfumo huo kwa ufanisi kusudi uweze kuendana na malengo yaliyokusudiwa.
Meje Jenerali Mzee amesema, katika utekelezaji wa mfumo huo kuna changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza ikiwemo mtandao wa simu, magari, wataalam hivyo jukumu la viongozi ni kutafuta suluhisho la utatuzi wa changamoto hizo kusudi kuwezesha ufanisi kwa walengwa kuweza kuwasaidia.
"Mpango huu unalenga kuondoa changamoto ya usafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ambapo wananchi watamsafirisha mama mjamzito kwenda kupata huduma na watapata malipo yao.
"Niwaombe wananchi wajipange kuupokea vyema, kwani unakwenda kuondoa changamoto ya vifo na kuhakikisha usalama wa mama na mtoto sote tunajua kubooresha huduma ya mama na mtoto ni huduma muhimu yenye baraka, kwa hiyo kina mama wanatakiwa kubeba mimba salama na kujifungua salama hasa katika vituo vya kutolea huduma," amesema Meja Jenerali Mzee.
Aidha, ameagiza wakuu wa Wilaya na Viongozi wengine katika maeneo yao kujipanga kuainisha waratibu wa huduma za dharura na mambo muhimu yatakayowezesha ufanikishaji wa M-mama katika kuhakikisha kina mama wanajifungua salama pamoja na watoto katika kuokoa maisha yao.
Mpango huo wa usafirishaji wa dharura Mobile Mama (M-mama ulizinduliwa mwaka jana jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto na kwa sasa unatekelezwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake Dkt. Yahya Hussein kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) amesema, shughuli zitakazofanyika katika Mkoa wa Mara ni pamoja na kutambua mkataba wa makubaliano kati ya mkurugenzi na madereva ngazi ya jamii, mafunzo ya mfumo wa M-mama kwa watoa huduma kuchagua waratibu na kutambua waratibu wa huduma za dharura.
Ambapo amesema kwamba, mteja wa kwanza kupata huduma hiyo ni baada ya miezi mitatu na kwa sasa pia watafanya utaratibu wa kuwatambua watu wenye magari katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara kusudi watakapoanza utekelezaji pasiwepo na kipingamizi.
Leah Daniel ambaye ni Mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto Mkoa wa Mara amesema, Mkoa wa Mara una vituo vinavyotoa huduma za upasuaji 35 magari ya kubebea magonjwa 13 na kwamba mahudhurio ya kliniki kwa wajawazito chini ya wiki 12 umeongezeka kutoka asilimia 13 mwaka 2017 hadi asilimia 39 mwaka jana. Huku lengo la kitaifa likiwa ni asilimia 45.
Amesema, upande wa uzazi wa mpango lengo la kitaifa ni asilimia 60 ambapo mkoa kwa sasa ni asilimia 34. Huku huduma za kujifungua kwa mwaka 2022 wanawake 93,539 walijifungua kituoni sawa na asilimia 98.4, na asilimia 1.6 walijifungua nje ya kituo.
Ameongeza kuwa, waliojifungua kabla ya kufika kituoni kwa mwaka 2022 ni 1,008. Wazazi waliojifungua nyumbani 344, na waliozalishwa kwa wakunga wa jadi 131.
Amesema, mkoa umefanikiwa kupiga hatua kwa kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito kutoka vifo 58 kwa mwaka 2017 hadi vifo 46 kwa mwaka 2022, huku vifo vya watoto kwa mwaka 2017 vilikuwa ni 1,306 hadi kufikia vifo 664 kwa mwaka 2022.
"Sababu za vifo za wajawazito ni pamoja na kumwaga damu, shinikizo la damu, upungufu wa damu, dawa za usingizi na sababu nyinginezo. Na vifo vya watoto vikisababishwa na mtoto kushindwa kupumua, matatizo yatokanayo na mtoto kuzaliwa njiti, kifafa cha mimba, kuvuja damu kabla ya kujifungua na watoto kufia tumboni,"amesema.