NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ametoa agizo kwa Maafisa Tarafa na Kata kusimamia na kuhamasisha kampeni ya upandaji miti kwenye maeneo yao ili kutunza mazingira.
Katika kuhakikisha kampeni ya urejeshaji uoto wa asili mkoani Rukwa inafanikwa Sendiga amezitaka halmashauri za Nkasi, Manispaa ya Sumbawanga, Kalambo na Sumbawanga kuboresha sheria ndogo ili ziweze kuchua hatua kwa waharibifu wa vyanzo vya maji.
Sendiga alisema mkoa huo una changamoto ya utapiamlo ,hivyo sasa ni wakati wa wananchi kupanda miti ikiwemo ya matunda ili kuimarisha lishe ya familia.

Kwa upande Mwenyekiti wa CCM Rukwa Silafu Maufi aliyeshiriki zoezi hilo alisema zoezi hilo la upandaji miti lililofanywa na viongozi wa Rukwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwa linapaswa kuwa endelevu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Jane Nyamsenda alisema programu ya upandaji miti iliyozinduliwa itakuwa utamaduni kwa wananchi wa Sumbawanga na kuwa itasaidia kurejesha uoto wa asili unaopotea kwa kasi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Manispaa ya Sumbawanga ilionesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Desemba 2022 hadi Januari 2023 jumla ya miche 250,190 imepandwa kati ya lengo la miti Milioni Moja na Laki Tano.