Saudi Arabia yatuma misaada zaidi kwa waathirika wa tetemeko la ardhi

GAZIANTEP-Februari 11, 2023 ndege ya sita ya misaada ya Saudi Arabia iliwasili Gaziantep nchini Uturuki ikiwa na tani 98 za misaada ambayo inajumuisha vyakula, mahema, mablanketi, mazulia na vifaa vya matibabu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la SPA, msaada huo unatolewa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mlinzi wa Misikiti Miwili Mitakatifu Mfalme Salman na Mwana Mfalme na Waziri Mkuu Mohammed Bin Salman.

Ndege ya misaada ya Saudi Arabua ilitumwa na Kituo cha Msaada wa Kibinadamu na Msaada wa Mfalme Salman (KSrelief) kwa maeneo yaliyoathiriwa na matetemeko ya ardhi nchini Syria na Uturuki kutekeleza jukumu la kibinadamu lililoelekezwa na Ufalme wa Saudi Arabia.

Katika hatua nyingine,DW iliripoti kuwa, juhudi za uokoaji zinaendelea kufanyika wakati idadi ya vifo vilivyosababishwa na janga hilo la asili imepanda na kufikia watu 24,000 huku mamia kwa maelfu wengine wamepoteza maeneo ya kuishi.

Sehemu kubwa ya vifo na athari mbaya ya tetemeko hilo la ardhi la siku ya Jumatatu imeshuhudiwa kwenye mji wa Mashariki mwa Uturuki wa Kahramanmaras.

Mji huo ndiyo ulitikishwa vibaya na janga hilo la asili ambalo liliporomosha majengo, kuharibu miundombinu na kuvuruga kabisa maisha ya watu ambao hadi Jumapili iliyopita walikuwa wakiishi maisha ya kawaida kwenye eneo hilo.

Mji huo unapatikana kwenye mkoa wa pembezoni kabisa mwa Uturuki ambao umekuwa makaazi ya watu waliokimbia machafuko ndani ya Uturuki na nchi jirani ya Syria.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa karibu watu 870,000 hivi sasa wanahitaji msaada wa haraka wa chakula nchini Uturuki na Syria. Nchini Syria pekee, watu wasiopungua milioni 5.3 huenda wamepoteza maeneo yao ya makaazi.

Watu bado waendelea kupatikana chini ya vifusi wakiwa hai. Kwenye maeneo ya maafa, miujiza imeendelea kushuhudia hata baada ya zaidi ya saa 100 tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Richter.

Mwanamke mmoja mjamzito kwa jina la Zahide Kaya amepatikana akiwa hai kutoka kwenye kifusi cha jengo baada ya saa 115 tangu kutokea kwa tetemeko.

Kulingana na shirika la habari la Uturuki, mwanamke huyo ameokolewa kwenye wilaya ya Nurdagi iliyopo katika jimbo la Gaziantep, Kusini Mashariki mwa Uturuki.

Mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka sita naye aliokolewa kutoka kwenye vifusi saa moja baadaye. Mama huyo amekutwa na majereha kadhaa mwili na alipelekwa mara moja hospitali.

Hata hivyo, hali ya hewa ya baridi kali imesababisha ugumu wa maisha kwa wale walionusurika na hata vikosi vya waokoaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news