NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan umeweka historia kubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo.
Ni baada ya kufanya uwekezaji wa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mbili zilizotokana na miradi ya Uviko-19 kwa ajili ya ujenzi wa jengo na ununuzi wa Mashine ya CT Scan ambao umesaidia kwa asilimia kubwa kuwapunguzia mzigo wananchi waliokuwa wakifuata huduma hiyo mikoa mengine.
Mkuu wa Idara ya Kitendo cha Mionzi na Picha katika Hospitali hiyo , Dkt.Goodluck Mbwilo amesema kwamba wanaishukuru Serikali kwa uwekezaji huo mkubwa ambao umeandika historia kwa mkoa huo ambapo awali hawakuwahi kuwa na mashine kama hiyo kutokana na kwamba mashine hizo zilikuwa zikipatikana kwenye hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa.
Amesema, kwenye hospitali hizo ndio zilikuwa zikipatikana lakini kwa sasa kila hospitali ya mkoa kupitia Rais Dkt Samia ameweza kufanikisha hilo na hiyo itasaidia kutoa huduma bora kwa watanzania wakiwemo wagonjwa wa ajali na wenye matatizo ambao wanahitaji huduma ya CT Scan kwa ajili ya uchunguzi.
Aidha, amesema kwamba awali wagonjwa walikuwa wakipata rufaa kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili au Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako huko napo gharama zilikuwa ni kubwa sana hivyo kwa sasa huduma hiyo inapatikana kwenye hospitali ya Bombo hivyo wananchi wachangamkie fursa hiyo kwa kuweza kupata matibabu na kuokoa gharama kubwa ambazo awali walikuwa wakizitumia.
“Kwa kweli tunaishukuru Serikali ya awamu yaa Sita kwa uwekezaji huu mkubwa ambao awali haukuwepo haya ni mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya kwa mkoa wetu hivyo niwaombe wananchi watumie fursa hiyo kujitokeza kuweza kuja kupata vipimo,”amesema.
Hata hivyo, amesema kwa sababu gharama za vipimo zipo chini ukilinganisha na hospitali binafasi huku akiwashauri watanzania hususani wakazi wa Mkoa wa Tanga na mikoa mengine kuchangamkia mpango wa fursa ya kuwa na bima ya afya ili kuwarahisishia kupata huduma za matibabu pindi wanapokuwa wakiugua.
Awali akizungumza Mteknolojia Mionzi katika Hospitali hiyo, Athumani Rajabu amesema mashine kubwa waliyoipata ina uwezo mkubwa inaweza kufanya uchunguzi kwa wagonjwa zaidi ya 100 kwa siku na Serikali imefanya kama zawadi kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga.