NA JAMES MWANAMYOTO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezielekeza taasisi zote za umma nchini kutumia mifumo shirikishi ya TEHAMA iliyoandaliwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) badala ya kutumia mifumo yao ambayo inajitegemea kiutendaji.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Arusha wakati akifunga Kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao kilichowashirikisha wadau zaidi ya 1500 wa serikali mtandao nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na washiriki wa kikao kazi cha tatu cha serikali mtandao wakati akifunga kikao kazi hicho jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
“Tumekubaliana mifumo yote ya TEHAMA iliyojengwa na itakayojengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao ni lazima iwe endelevu ili iwe na tija kiutendaji hivyo taasisi zote za umma hazina budi kutumia mifumo hiyo shirikishi ya TEHAMA,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa ni lazima kwa kila taasisi ya umma kuhakikisha sheria na miongozo ya serikali mtandao inazingatiwa wakati wa kusanifu mifumo ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na kuomba kibali Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ili kupata idhini ya kutengeneza mifumo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema ofisi yake imejipanga kuhakikisha eGA inasimamia vema matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma na inajenga mifumo jumuishi inayowasiliana ili kurahisisha utendaji kazi katika utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa, washiriki wa kikao kazi hicho wametoa maoni na mapendekezo ya namna ya kuimarisha serikali mtandao na kushauri uboreshaji wa baadhi ya mifumo inayotoa huduma kwa umma pamoja ili kupanua wigo wa utoaji wa huduma mtandao, hivyo mamlaka yake itahakikisha inayafanyia ushauri, maoni na mapendekezo yaliyotolewa kwa lengo la kuboresha matumizi ya serikali mtandao nchini.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao, Dkt. Jasmine Tiisekwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa agizo lake la kuimarisha Serikali Mtandao nchini ikiwa ni pamoja na utashi wake wa kisiasa wa kuijenga Tanzania kuwa ya kidijitali.
Kaulimbiu ya kikao kazi hicho cha tatu cha Serikali Mtandao ni ‘Mifumo Jumuishi ya TEHAMA kwa Utoaji Bora wa Huduma za Umma’.