NA OR-TAMISEMI
WAGANGA wakuu wa halmashauri zote nchini wamehimizwa kuhamasisha utolewaji wa matone ya Vitamin A kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Hatua hiyo imetajwa kuwa, itasaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuzuia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyosababishwa na ulaji duni wa vyakula mchanganyiko.
Rai hiyo imetolewa Februari Mosi, 2023 na Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Bi.Asiatu Mbwambo wakati wa kikao kazi cha timu ya usimamizi shirikishi kutoka OR-TAMISEMI na watoa huduma wa kituo cha afya Matemanga kilichopo wilayani Tunduru.
Alisema, msingi wa lishe unaitaka watoto chini ya miaka mitano kula vyakula mchanganyiko lakini milo ambayo wanapewa watoto haikidhu makundi matano ya vyakula.
"Watoto wanatakiwa kula vyakula mchanganyiko, lakini milo yetu haikidhi aina ya vyakula kutoka makundi matano ya vyakula kwa hiyo matone ya Vitamin A yana vitamins zinazosaidia kuboresha afya na kuimarisha ukuaji wa mtoto.
"Upungufu wa Vitamin A mwilini unaweza kusababishwa na uwepo wa maradhi ingawa sababu kuu ni ulaji wa vyakula visivyo na Vitamin A ya kutosha,"amesema Mbwambo.
Amesema kuwa, utolewaji wa matone ya Vitamin A kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuboresha afya za watoto baada ya tafiti kuonesha kwamba upungufu wa Vitamin A kwa watoto huchangiwa pia na ulaji duni.
Mbwambo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto walio chini ya miaka mitano kuhakikisha wanawapeleka watoto kupata matone ya Vitamin A katika kampeni zinazofanyika kila mwezi Juni na Desemba nchi nzima.