NA DIRAMAKINI
WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika, Simba SC wamefufua matumaini yao ya kutinga hatua ya nane bora ya ligi hiyo baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vipers.
Timu hizo mbili zimekutana jioni ya Februari 25, 2025 kwenye Uwanja wa St.Mary’s jijini Kampala, Uganda huku Simba ikiambulia ushindi huo muhimu wa ugenini.
Inonga alipokea pasi iliyoandaliwa vyema kutoka kwa Moses Phiri aliyeshirikiana na Kibu Denis kwa sehemu ya mashambulizi ya Simba kabla ya kutolewa kipindi cha pili.
Baada ya bao hilo, Simba SC waliendelea kumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa huku wenyeji Vipers wakifanya mashambulizi ya haraka, lakini hata hivyo ilionekana Simba SC wapo makini kuwakabili.
Dakika 15 za kipindi cha pili Vipers walirudi kwa kasi na kuwashambulia Simba SC kwa kasi, lakini walionekana kuwa watulivu kuhakikisha hawafanyi makosa.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa wawakilishi hao wa ligi ya mabingwa ambao kabla ya hapo walishindwa mara mbili kutoka kwa Horoya na Raja Casablanca.
Wakati huo huo, kikosi cha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ kitawakaribisha Vipers kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi ijayo.
Siku hiyo, Simba watakuwa wanajaribu kutafuta ushindi wao wa kwanza nyumbani kwenye kampeni zinazoendelea za hatua ya makundi ili kuwavutia mashabiki wao na kurejesha furaha ambayo ilionekana kufifia awali.
Mbali na kukusanya alama tatu jijini Kampala, Simba itaweka mfukoni kitita cha shilingi milioni 5 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye aliahidi kununua kila bao litakalofungwa na wawakilishi hao wa Tanzania, Simba na Young Africans katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na Ligi ya Mabingwa barani Afrika.