Simba SC,Al Hilal watoana jasho Dar

NA DIRAMAKINI

MCHEZO wa kirafiki wa Kimataifa kati ya Simba SC ya jijini Dar es Salaam na Al Hilal (Al Hilal Omdurman) kutoka jijini Omdurman nchini Sudan imetamatika kwa miamba hao kutoka sare ya bao moja kwa moja.

Mtanage huo wa nguvu umepigwa Februari 5, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Ndani ya dakika sita, Makabi Lilepo aliwapatia Al Hilal bao baada kumalizia pasi ya mpira wa adhabu iliyopigwa na mlinzi wa kushoto, Ibrahima Emora.

Aidha, winga Augustine Okrah alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kupata maumivu ya msuli na kutolewa dakika ya 15 nafasi yake ikachukuliwa na Habib Kyombo.

Mshambuliaji Jean Baleke nae alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 33 baada ya kupata maumivu nafasi yake ikachukuliwa na nahodha John Bocco.

Kipindi cha pili, Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' alifanya mabadiliko kuwaingiza Clatous Chama, Pape Sakho, Mohamed Hussein Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Nassor Kapama na Mohamed Mussa kuchukua nafasi za Gadiel Michael, Peter Banda, Kibu Denis na Jimmyson Mwanuke, Erasto Nyoni, Ismael Sawadogo na Sakho

Baada ya mabadiliko hayo, Simba SC walionekana kuongeza kasi katika eneo la kushambulia ambapo Kyombo aliwasawazishia bao hilo dakika ya 81 kwa shuti kali ndani ya 18 akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Sakho.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Klabu ya Al Hilal, Mohamed Ibrahim alishuhudia mchezo huo wa kirafiki baada ya kuwasili mapema jijini Dar es Salaam akitokea Sudan.

Rais Mohamed alipokelewa na Mkurugenzi wa Mashindano na Wanachama, Mzee Hamisi Kisiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupelekwa moja kwa moja hotelini.

Baada ya kutua nchini Rais Mohamed aliushukuru uongozi wa klabu kwa kukubali kuipokea timu yake na anaamini maandalizi ya wiki moja waliopata ni mazuri ambayo yatawasaidia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tunaushukuru uongozi wa Simba kwa kukubali kutupokea na kusaidia kambi yetu ya maandalizi yetu. Simba ni timu kubwa tunaamini mchezo huu utampa kocha mwanga kuelekea mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns.

“Hali ya hewa ya Sudan ni sawa na hapa jijini Dar es Salaam, kwa hiyo wachezaji wetu wamepata maandalizi mazuri ya utulivu,”alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news