Tanzania yakabidhiwa jukumu la Kimataifa katika Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu

NA GODFREY NNKO

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imekabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu katika Jumuiya za Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 15,2023 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, uenyekiti huo ulikabidhiwa kwenye hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya jumuiya hiyo Februari 13, 2023 jijini Brussels, Ubelgiji.

"Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, kwenye Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya OACPS, Mheshimiwa Jestas Abuok Nyamanga alikabidhiwa rasmi uenyekiti wa sekta hiyo kwa ngazi ya mabalozi na Balozi wa Ghana nchini Ubelgiji, Mheshimiwa Harriet Sena Siaw-Boateng ambaye nchi yake imemaliza muda wa uenyekiti,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa Tanzania kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa sekta hiyo ulifikiwa katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa OACPS uliofanyika Juni, 2022 jijini Brussels nchini Ubelgiji.
Uenyekiti wa Tanzania utakuwa kwa ngazi mbili ambazo ni za mabalozi wa jumuiya waliopo Brussels na mawaziri wenye dhamana ya Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu ndani ya jumuiya na utadumu kwa miaka miwili hadi Februari, 2025.

"Tanzania katika kipindi chake imejipanga kikamilifu kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali katika jumuiya ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati madhubuti na mazingira ya kuwezesha wananchi kupitia nchi zao kunufaika ipasavyo na uchumi wa buluu ikiwemo uvuvi na rasilimali zingine za majini.

"Lengo ni kuchochea uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu, kujenga uwezo na matumizi bora ya sayansi na teknolojia na kuongeza wigo wa masoko kwa bidhaa zitokanazo na uvuvi na uchumi wa buluu, kupambana na uvuvi haramu na kuendeleza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo imefafanua kuwa, Tanzania katika kipindi husika itakuwa na jukumu la kuandaa Mkutano wa Mawaziri wa OACPS wenye dhamana ya masuala ya uvuvi ambao unatarajiwa kufanyika nchini mwaka 2024.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miongoni mwa sababu zilizopelekea Tanzania kuchaguliwa katika nafasi hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa ushawishi wake ndani ya Jumuiya ya OACPS na kuthamini utayari, dhamira na hatua thabiti zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuchochea na kusimamia masuala mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo yale yanayohusu sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news