NA MWANDISHI WETU
KAIMU Mkuu wa Chuo cha Ufundi VETA mkoani Mara, Mwalimu David Luis ameushukuru Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Tatu (TASAF) kwa jitihada inazozifanya kuwezasha vijana kupata ujuzi ambao utawasaidia kujiajiri au kuajiriwa ili waweze kuendesha maisha yao na familia pamoja na kujitoa kwenye janga la umaskini.



“TASAF walitulea vijana kumi na tatu ambao hapa chuoni wamegawanyika katika kozi tofauti ambapo katika fani ya kompyuta wapo vijana wanafunzi wanne, umeme wa majumbani wapo wanafunzi watano, fundi bomba yupo kijana mmoja, ufundi wa magari mwanafunzi mmoja, upande wa udereva pia kuna mwanafunzi mmoja,” amesema Mwalimu David.


Ameongeza kwamba TASAF waliwaletea kiasi cha fedha zaidi ya shilingi milioni 11 pesa ambazo wanufaika hao wanagharamiwa kwenye ada, nauli na chakula cha mchana wanapokuwa hapa chuoni kwa ajili ya mafunzo
Aidha, Mwalimu David amesema kwamba kuhusu changamoto ya mabweni katika chuo hicho tayari Serikali kupitia Bajeti ya fedha ya 2022/2023 ilishawapangia zaidi ya shilingi milioni 900 ambazo zimetegwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mabweni katika chuo hicho, lakini pia wana chuo kingine ambacho kipo katika hatua ya mwisho wilayani Butiama na tayari kina mabweni na kitakapokuwa tayari wataweza kupokea wanafunzi wengi zaidi.

Kwa upande wake Elly Maduhu ambaye ni mratibu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) mkoani Mara amesema kwamba, mwaka 2010 walibahatika kupata mradi wa TEA kupitia SDF walipewa kiasi cha shilingi milioni 80 ambazo waliweza kusajili wanafunzi 280 katika fani ya ufundi wa kompyuta na matumizi ya kompyuta, wanafunzi wote hao tayari wameshahitimu mafunzo yao na baadhi yao wameajiriwa na wengine wamejiajiri.
Ameongeza kwamba, kupitia TASAF waliweza pia kupata mradi kupitia kaya maskini ambapo wanafunzi kumi na tatu kati yao wanafunzi nane tayari wameanza mafunzo na wengine watawasili kwenye chuoni hapo muda si mrefu.


Mwanafunzi Asha Juma ambaye ni mnufaika na mradi wa TASAF pamoja na TEA ametumia nafasi hiyo kutoa shukurani zake kwani kupitia miradi hiyo ameweza kupata mafunzo ambayo yatamsaidia kuajiriwa au kujiajiri na kuendesha maisha yake ya baadae.
Naye Mabonera ambaye ni mwanafunzi wa ufundi Seremala katika chuo hicho ameishukuru TASAF na TEA kwa kumpatia ufadhili wa mafunzo ambapo amewashauri vijana wengine watakaopata nafasi kupitia miradi hiyo kuzitumia nafasi hizo kwa kujifunza kwa bidii kwa ajili ya manufaa yao ya baadae.
Afisa kutoka Dawati la Malalamiko TASAF akizungumza na wanafunzi katika moja ya madarasa ya chuo hicho ambapo amewaasa kusoma kwa bidii ili waweze kupata ujuzi ambao utawasaidia katika maisha yao mara watakapoondoka chuoni hapo nakuingia mtaani.


Mwanafunzi Asha Juma kutoka Mtaa wa Matare mjini Musoma ambaye anapata mafunzo ya ufundi bomba katika chuo hicho kwa upande wake ameishukuru TASAF kwa kumpatia nafasi ya kusoma katika chuo hicho ambapo ameahidi kutoichezea nafasi hiyo na kusoma kwa bidii ili kujikwamua katika hali ngumu ya maisha na umasikini kwa maisha yake ya baadaye.