TEF:Tunaishukuru Serikali kwa hii hatua

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kufanikisha kusomwa kwa mara ya kwanza Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari.

Muswada huo umesemwa leo Februari 10, 2023 bungeni jijini Dodoma huku Balile akisisitiza kuwa,wadau wa habari nchini wanaendelee kuamini waliyokubaliana yamo na siku za karibuni watakutana kwa mara nyingine baada ya kupata muswada huo ili waone kama waliyopendekeza yatakuwa yameingia.
Balile ameyasema hayo leo Februari 10, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akisema kuwa, ni jambo la faraja kuona kuwa, hata shughuli za Bunge kwa sasa zinaendeshwa mubashara.

"Leo Bunge limeisha, tumeona Muswada ulivyosomwa, Serikali imerejesha Bunge live na huko nyuma tuliambiwa kwamba Bunge likiwa live watu wanashindwa kufanya kazi na sisi tukasema hii hoja hapana. Haiwezekani mtu ana kazi ya kuendesha basi kwenda Iringa eti kwa sababu Bunge ni live akae nyumbani tu bila kuendesha basi.

"Unamuweka wapi mlinzi anayefanya kazi usiku kucha aangalie kinachoendelea, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais alirejesha Bunge live. Lakini haya hatusemi Rais pekee pia Mheshimiwa Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojiaya Habari) kwa mambo mengi tulikuwa tukivutana na wataalam.

"Tulikuwa hatujawahi kusema, tulisema mambo yanakwenda vizuri sana, kumbe moyoni tulikuwa tunaugulia maumivu, unajiuliza kwa nini mtu anapinga hoja iliyokubalika ulimwenguni kote hupati jibu.

"Kikao cha Novemba 21, 2022 Mheshimiwa Waziri kwa kweli alisimamia vilivyo alihakikisha yale yaliyokuwa magumu yanapata suluhisho. Muswada umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni leo, hatujapata nakala ya muswada kujiridhisha yaliyomo, lakini kwa yale tuliyokubaliana tunaamini yatakuwa yote yameingia,"amefafanua Balile.

Katika hatua nyingine,Mwenyekiti wa TEF amebainisha kuwa,Mheshimiwa Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojiaya Habari amekuwa mlezi mzuri na amekuwa akionesha ushirikiano wa hali ya juu.

"Ila hapa mwisho Mkurugenzi wake alisema lisilo sahihi na si la kisheria, sisi tulikuwa na wajibu wa kuweka mwongozo wa kisheria na usahihi wa jambo hili.

"Tunamshukuru pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Feleshi (Mheshimiwa Jaji Dkt.Eliezer Mbuki Feleshi) kwa kweli muda wote ameonesha kwamba anapenda nchi hii iwe na sheria ambazo zina uhuru kidogo wa habari. Kwa kweli wanaungana na Mheshimiwa Rais juu ya jambo hili,"amefafanua Balile.

Amefafanua kuwa, kwa mwaka 2016 Tanzania katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ilipanda mpaka nafasi ya 71, lakini ghafla ikaporomoka mpaka nafasi ya 124 mwaka 2019/2020, mwaka jana ikapanda kidogo na mwaka huu tumekuwa 123.

"Tunajiuliza kwa nini tumeporomoka zaidi wakati nchi nyingine zimepanda na sisi hapa hatupiganii kwamba wahariri au waandishi peke yao. Bali tunapigania haki ya msingi inayowezesha haki nyingine kupatikana.
"Vyombo vya habari vikiandika jambo mfano yule daktari aliyemfumua mtu mshono kwa kushindwa kulipa gharama shilingi 10,000 tunaona matokeo.

"Lile tukio, vyombo vya habari vilipotangaza tu tuliona Waziri wa Afya alikimbia haraka na kuwaeleza Baraza la Madaktari Tanganyika washughulike naye, na ndani ya saa 24 walishughulika naye na yule mtu aliyefumuliwa akashonwa. Kwa hiyo vyombo vya habari viliwezesha haki ya matibabu.

"Mifano ni mingi, tumekuwa tukiona vikiripoti juu ya rushwa na hatua zinachukuliwa. Kwa hiyo baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ndogo ndogo tunaamini utaingia kwenye website ya Bunge, tutaanza kuujadili na kwa pamoja tutaona je?

Yaliyomo yanatusaidia kwenye taifa lililo moja kuwa na nchi ambayo watu wake mawazo yao yanaheshimika na kusikilizwa.

"Sisi tunasema tunapigania hii haki ya uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari si kwa sababu ya vyombo vya habari peke yake bali kwa ajili ya Watanzania wote. Sasa utakuwa mwanzo na chimbuko la ukuaji wa demokrasia nchini kuwezesha kutoa mawazo, ustaarabu katika nchi yetu na wakati mwingine itapelekea katika misingi ya utawala bora na utawala wa sheria,"amebainisha Balile.

Pia amesema, kama hakuna mawasiliano mazuri tutajikuta mtu anafanya atakalo. "Tunapenda sana kumshumuru Mheshimiwa Rais, hatujui yeye kaelekeza, lakini kwa kauli ya Msemaji Mkuu wa Serikali kasema linakwenda Aprili halafu tukasikia Waziri amesema hapana ni kesho. Tunamshukuru sana tunauona mkono wake.

"Nivishukuru vyombo vya habari vimekuwa kwenye mapambano muda wote kudai uhuru wa vyombo vya habari na uhuru,lakini ukiangalia habari zilizochapishwa na kutangaza kwenye TV, Radio na mitandao ya kijamii tumeshirikiana sana.

"Pia, nizishukuru taasisi mbalimbali za kihabari zilivyoshirikiana kwa hatua moja ama nyingine kutoa mafunzo, uchechemuzi kwa kweli tumekuwa na ushirikiano mkubwa na mzuri sana kuliko 2015/2016 wakati tunapambania kwa mara ya kwanza ilipotungwa hii sheria.
"Sisi tutashirikiana na wadau wote, wafadhili, taasisi za kiserikali na wote wanaoweza hatutaweza kumuacha mtu yeyote nyuma kufanikisha upatikanaji wa sheria nzuri.

"Mheshimiwa Waziri asiwe na wasiwasi, tutaendelea kushirikiana naye na leo nitampigia simu lengo letu kubwa ilikuwa sheria hii iingie bungeni ili tuweze kupata sheria bora,"amefafanua Balile.

Mzee Salim

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim amesema, kuna thamani kubwa ya kuwa na Taifa lwa watu wenye uhuru wa kujieleza ukiwemo uhuru wa kutosha wa vyombo vya habari.

"Watanzania wawe na a talking nation, Taifa la watu wanaosema, ukiwa unatoa uhuru wa kujieleza panaweza kuwa na tofauti kati ya mtu na mtu anayetafsiri, lakini unaposikia sauti ya huyu na huyu ndio Utawala bora tunakwenda katika demokrasia.

"Taarifa yetu haikulenga kulaumu mtu yeyote, isipokuwa ni kutoa hisia za jukwaa kwa niaba ya wahariri kwamba hatukufurahishwa kila siku kuambiwa ngoja...ngoja na tulikuwa tunachelea safari hii tukiambiwa ngoja kesho kutwa kinakuja kikao cha bajeti.

"Lakini matumaini yetu yaliyopimwa yamepita tunasonga mbele, tutashirikiana kwani sote tunataka kuijenga nchi yetu,"amefafanua Mzee Salim.

Akilimali

Angela Akilimali, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ameishukuru Serikali kwa kuwezesha kusomwa kwa mara ya kwanza muswada huo.

"Nashukuru kwa muswada huu kusomwa kwa mara ya kwanza, natumaini yale ambayo tunatarajia waandishi wa habari tukiwa kazini sasa tutaweza kuanza kuona maisha bora kwa waandishi wa habari. Kwa sababu mara nyingi wanahabari tumekuwa nyuma, lakini tukiwa na kanuni nzuri, sheria nzuri kila kitu kitakwenda sawa.

"Tulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania na wadau wote waliochangia na waandishi wa habari kulisemea jambo hili na hatimaye kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita mswaada huu umeweza kusomwa bungeni,"amefafanua Akilimali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news