NA OR-TAMISEMI
TIMU ya Usimamizi Shirikishi kutoka Idara ya Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imetoa wito kwa timu za uendeshaji wa huduma za afya Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha inaimarisha na kusimamia utoaji wa huduma bora za afya katika vituo vya kutolea huduma.
Wito huo umetolewa Januari 31,2023 na Mkurugenzi wa Huduma za Afya,Lishe na Ustawi wa Jamii OR-TAMISEMI, Dkt.Ntuli Kapologwe alipozungumza kwa niaba ya timu ya usimamizi shirikishi kutoka OR-TAMISEMI katika kikao kazi kati ya timu hiyo na timu ya uendeshaji wa huduma za afya Mkoa wa Ruvuma.
Amesema kuwa, jukumu pekee la watoa huduma za afya nchini ni kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya nchini vinahudumia wananchi saa 24 na kutoa huduma bora za afya ili kwenda sambamba na nia ya Serikali ya kusogeza huduma hiyo katika jamii.
Sambamba na hilo Kapologwe ameitaka timu hiyo kuhakikisha inasimamia ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya akisisitiza kuwa mapato hayo yatumike katika kuboresha utoaji wa huduma ya afya ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma.
Pamoja na kikao hiko timu hiyo ilitembelea na kukagua utoaji wa huduma za afya pamoja na utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Vituo vya Afya Lilambo, Masigira pamoja na Mletele vilvyopo katika Manispaa ya Songea.
Timu imemshauri Mganga mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha kuwa huduma ya mama na mtoto inaanza kutolewa katika kituo cha afya Lilambo kuanzia Februari 25,2023.
Aidha, timu hiyo imetoa wito kwa Waganga Wakuu wa Halmashauri Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha Vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinatoa huduma ya chanjo katika maeneo ambayo yapo mbali na vituo vya afya ( huduma za mkoba) ili kuwapunguzia wananchi adha na gharama ya kufuata huduma hiyo vituoni hapo.