NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini mkoani Mara, kuwa waaminifu na kuachana na tabia za utoroshaji madini ambayo baadhi ya wachimbaji wamedaiwa kujihusisha nayo.
Akizungumza katika mafunzo ya siku mbili kwa wachimbaji wadogo wadogo mkoani humo,Profesa Kikula alisema, lengo ni kuhakikisha shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini zinafanyika kwa kuzingatia usalama,afya na utunzaji wa mazingira kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na serikali.
Kikula amewataka wachimbaji hao kuzingatia mienendo na sheria za uchimbaji ikiwemo kuepukana na vitendo vya utoroshaji wa madini, na kufuata sheria za madini pia shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira ikiwemo utumiaji wa baruti, leseni za madini na biashara ya madini katika uendeshaji wa shughuli hizo kwa wachimbaji wadogo wadogo.
"Kila mmoja anatambua jinsi shughuli za madini zilivyo na manufaa kwa wachimbaji na wananchi pamoja na taifa kwa ujumla, hivyo ni vyema tuendelea kuchimba kwa uadilifu na kutovunja sheria zetu za madini ilituendelee kupata fursa zaidi na kwa vizazi vijavyo,"alisema.
Nao baadhi ya wachimbaji wadogo wadogo wa madini mkoani humo,wameishukuru serikali kwa kutoa mafunzo hayo, kwani yatawasaidia katika kujikinga na kuchukua tahadhari pindi wanapokuwa katika shughuli za uchimbaji, pia wameiomba serikali kuwapunguzia tozo za viroba za zaidi ya mara mbili zinazotozwa na halmashauri kutokana na kuwa kikwazo kwao.
Wambura alisema wamekuwa wakitozwa ushuru wa shilingi 1000 kwa kila kiroba ikiwa ni baada tu ya kutoka mgodini, pesa ya huduma ya mapato (service revenue) ambacho awali hakikuwepo, hivyo kupelekea kushindwa kufikia lengo na hata kushuka na kushindwa kuendelea kujikita na uchimbaji.
Alisema, tozo hizo zimekuwa ni changamoto kubwa ambazo baadhi wanashindwa kufahamu ni kwa namna gani wanaweza kuondokana nazo pamoja na kujitahidi kujikwamua kutoka katika wimbi la umasikini.
"Unalazimika kutoa shilingi 1000 kwa kila kiroba cha mawe baada ya kutoa mgodini (duarani) na huelewi baada ya uchenjuaji ni kiasi gani cha dhahabu unaweza kupata na hapo tayari umeshatoa ushuru zaidi ya mara mbili tunaomba serikali iingilie kati suala hili,"alisema.
Nae Katibu Msaidizi wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Mara (MAREMA), Deogradius Chungula alisema, serikali inapoenda kutatua suala la tozo za mara mbili pia iangalie na upande wa nishati ya umeme katika migodi kwani wamekuwa wakilazimika kutumia mafuta ya petroli na dizeli ili kuweza kuboresha shughuli zao.