'Tumesimama imara katika umoja kuhubiri injili wakati wote ufaao na wakati usiofaa'

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT), Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala amesema, injili itaendelea kuhubiriwa muda wote huku wakiendelea kuimarisha umoja wao kwa kusudi hilo hilo la kuujenga Ufalme wa Mungu kupitia neno na maombi.

Rejea, 2Timotheo 4:2-5 Biblia inasema, "lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.

"Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti, nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako."

Rais Dkt.Nabiijoshua ameyabainisha hayo baada ya kushiriki kikao cha mitume na manabii katika mikoa ya Dar es Salaan na Pwani ambapo pia Katibu Mkuu wa umoja huo, Justine Kalebu alishiriki.

Dhamira ya umoja huo ambao unalenga kuwaleta pamoja mitume na manabii kwa ajili ya kueneza habari njema ya neno la Mungu nchini, kuombea, kuwezeshana, kuwezesha wenye mahitaji mbalimbali pia umekusudia kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Hivi karibuni,Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania alitwaa asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa nafasi ya urais katika Umoja wa Manabii na Mitume nchini Tanzania (Unity of Apostles and Prophets Tanzania).

Ushindi huo ulitokana na kura 179 alizopata huku akiwaacha mbali washindani wake akiwemo Mchungaji Ceasar Masisi aliyepata kura 42 na Mtume Joackim Kimanza aliyepata kura nne kupitia uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Anatoglo uliopo Ilala, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Askofu Profesa Rejoice Ndalima alimtangaza rasmi Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala kuwa Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii nchini Tanzania.

Aidha, mitume na manabii mbalimbali nchini walionesha imani kubwa juu ya Dkt.Nabiijoshua huku wakimpongeza na kuahidi kumpa ushirikiano mkubwa aweze kutekeleza jukumu lake la kuwaunganisha viongozi hao wa kiroho ili waweze kulihubiri neno la Mungu kwa ufanisi nchini

Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) unaongozwa na Rais Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yenye makao yake makuu mjini Morogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news