TUWAHESHIMU WALIMU:Waziri Mkuu wetu, kweli amesema vema

NA LWAGA MWAMBANDE

FEBRUARI 2, 2023 bungeni jijini Dodoma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema, wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kwa karibu na walimu katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kuwafundisha, kuwalea, kuwaongoza na kuwaendeleza wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, mila, desturi na tamaduni za Kitanzania.

Pia amesema kuwa, walimu wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana kuliko mapungufu machache tunayoyaona hasa kupitia mitandao ya kijamii. Walimu wamekuwa wakifundisha, wakilea vijana wetu katika mazingira tofauti pamoja na kutoa huduma mbalimbali ambazo nyingine zilitakiwa kutolewa na wazazi au walezi.

“Bahati mbaya kwa jamii zetu ni kuwa, jambo baya husambaa kwa haraka zaidi kuliko jema. Hata hivyo, licha ya mapungufu kutoka kwa baadhi ya walimu kama nilivyoainisha, walimu wetu wanafanya mambo mengi na makubwa ya kimalezi kwa watoto wetu ambayo pengine hayasambazwi na kuonekana.”

Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa jamii kutobeza juhudi zinazofanywa na walimu wetu badala yake tuwatie moyo, hasa wale wanaozingatia miiko ya taaluma zao na misingi ya malezi. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, walimu wana nafasi muhimu sana katika familia, jamii na Taifa letu kwa ujumla. Endelea;


1:Kweli tulishaelezwa, jinsi ubaya huvuma,
Ndivyo tunavyozoezwa, kwamba tusione mema,
Jinsi ubaya wakuzwa, na kusababisha noma,
Tuwaheshimu walimu, inafaa kuwaenzi.

2:Yatokea matukio, machache yasiyo mema,
Watu huko ni vilio, kusukumiza lawama,
Ya kwamba walimu ndio, wanaofanya unyama,
Tuwaheshimu walimu, inafaa tuwaenzi.

3:Hata kwa jamii zetu, walio wengi ni wema,
Wachache yao ni kutu, eti ndio wanavuma,
Huchafua utu wetu, sote twavaa lawama,
Tuwaheshimu walimu, inafaa tuwaenzi.

4:Walimu ndio walezi, watoto wanaosoma,
Wanafanya kubwa kazi, watoto wanasimama,
Ni wachache wapuuzi, tusizikuze lawama,
Tuwaheshimu walimu, inafaa tuwaenzi.

5:Hao hasa ni wapishi, wakitoa taaluma,
Sawasawa wanajeshi, akili zikae vema,
Tusitekwe na uzushi, walimu wengi ni wema,
Tuwaheshimu walimu, inafaa kuwaenzi.

6:Walimu Hongera sana, kazi mfanyayo njema,.
Mwaelimisha vijana, hadi wanakua vyema,
Sasa ndio twawaona, wanafanya kazi njema,
Tuwaheshimu walimu, inafaa kuwaenzi.

7:Walimu mmetufaa, na sisi watu wazima,.
Kwrnu ndio tulikaa, tukajua na kusoma,
Sisi ndio tunafaa, nyie tuwasrme vema,
Tuwaheshimu walimu, inafaa kuwaenzi.

8:Waziri mkuu wetu, kweli amesema vema,
Tusibeze watu wetu, walimu wengi ni wema,
Wafanyao mambo butu, namba waweze zisoma,
Tuwaheshimu walimu, inafaa tuwaenzi.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767224602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news