Ukeketaji haukubaliki, HGWT yawaeleza wanafunzi Serengeti

NA FRESHA KINASA

KATIKA kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupinga ukeketaji wa watoto wa kike na wanawake ambayo hufanyika Februari 6, ya kila mwaka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalopambana na ukatili wa kijinsia mkoani Mara limetoa elimu ya madhara ya ukeketaji na ukatili mbalimbali kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Serengeti iliyopo Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti mkoani Mara.
Ambapo kauli mbiu ya siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji wa watoto wa kike kwa mwaka huu inasema, "wanaume na wavulana tushirikiane kupinga mila na desturi zenye madhara ili kutokomeza ukeketaji."

Shirika hilo limewataka wanafunzi hao kuendekea kuwa chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuwa mabalozi wa kupaza sauti kupinga mila hiyo na kutoa elimu kwa wengine hasa katika Wilaya ya Serengeti, Tarime na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mara ambapo suala hilo limekuwa likifanyika licha ya Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kulivalia njuga.

Ukeketaji hufanywa na koo za kabila la Kikurya kila ufikapo msimu wa tohara kwa wasichana hasa mwezi Desemba na wanafunzi wanapokuwa likizo kama sehemu ya kudumisha mila yao.
Ambapo Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limekuwa likipambana na ukeketaji na pia linatoa huduma ya hifadhi wa wasichana wanaokimbia ukeketaji kutoka katika familia zao kupitia vituo vyake vya "Hope Mugumu Nyumba salama na Nyumba Salama Kiabakari" chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly.

Afisa Mwelimishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuel Goodluck amefanya mazungumzo na DIRAMAKINI ambapo amesema, kupitia elimu hiyo anaaminj itawasaidia wanafunzi hao kutambua madhara ya ukeketaji na pia watahusika kutoa elimu hiyo katika maeneo yao sbamba na kushiriki kuwatetea watoto wa kike ambao ndio wamekuwa wakikumbana na kadhia hiyo na kupelekea baadhi yao kukatisha masomo yao.

"Sisi tunaendelea kutoa elimu tukiamini kwamba elimu ni njia muhimu ya kulimaliza jambo hili. Tunawapa elimu watoto hawa tukitambua kwamba watakuwa sehemu ya kuisaidia serikali pamoja na wadau mbalimbali ambao wapo katika mapambano ya ukeketaji. Niiombe Serikali,wadau pamoja na jamii kwa ujumla tushiriki katika kutokomeza kwa kuweka mikakati madhubuti kwa kuwafikia wazee wa mila, wanasiasa,viongozi wa dini ili kwa pamoja tushiriki,"amesema Goodluck.
"Wanaofanya ukeketaji wapo katika jamii, tunawafahamu na pia tunao wazee wa kimila ambao wana mchango wa kusaidia mapambano haya kwa hiyo niombe kwamba wanaobainika wawajibishwe na pia jamii iwafichue mbele ya vyombo vya sheria wanaofanya mila hii kwa siri,"amesema na kuongeza kuwa.

"Sote tunajua ukeketaji ni kosa kisheria na ni kinyume cha haki za binadamu kitendo hiki kina madhara ikiwemo kuwaathiri watoto kisaikolojia, kukatisha masomo yao, kukosa kujiamini, na hata kuwaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kutokana na kutumia kifaa kimoja wakati wa kukeketa na hakuna umakini wowote unaotumika,"amesema Goodluck.

Aidha, Goodluck ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Mara kwa jinsi inavyolivalia njuga kuhakikisha inakabiliana na ukeketaji ambapo amesema juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono wa makundi yote wakiwemo wananchi, wanasiasa, viongozi wa dini kwani linarudisha nyuma maendeleo na kuwafanya watoto wa kike waendelee kuwa wahanga wa mila hiyo ambayo kim-singi imepitwa na wakati.

Bhoke Chacha ni mwanafunzi katika Shule ya Sekondari Serengeti ambapo amelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa hatua ya kutoa elimu kwa wanafunzi shuleni hapo ya madhara ya ukeketaji na kuwapa hamasa vijana kusimama kidete kupinga ukeketaji. Ambapo pia ameiomba Serikali kuwawajibisha vikali wanaokutwa na hatia Kama njia ya kutoa fundisho kwa wengine.

"Serikali imekiwa ikichukua hatua kali kukabiliana na watu wanaokutwa na madawa ya kulevya pamoja na nyara za serikali. Natambua Serikali ni mkono mrefu tena wenye nguvu uzidishe hatua kali kwa ngariba wanao kamatwa pamoja na wote wanaofanya mila hii. Na pia niiombe jamii kutoa ushahidi mahakamani wanapokamatwa wahusika kusudi wawajibishwe kwani bila ushahidi kutolewa watoto wa kike watakeketwa na bado hakuna mtu atakayefungwa jela,"amesema Bhoke Chacha.
Zacharia Ephania ameomba vijana wa kiume na wanaume kuwa na msimamo wa kuacha kuoa mabinti waliokeketwa kwani itasaidia kumaliza tatizo hilo. Huku akiomba elimu iendelee kutolewa zaidi kwa makundi mbalimbali kwa njia ya mikutano ya hadhara, makongamano na matamasha mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news