NA FRESHA KINASA
SHIRIKA la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara limetoa mafunzo ya mifumo ya uongozi na utawala kwa wajumbe wa bodi ya shirika hilo pamoja na watumishi ili watambue majukumu yao kikamikifu katika kuleta ufanisi na tija.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Februari 3, 2023 Meneja wa shirika hilo (VIFAFIO), Majura Maingu amesema, lengo ni kuhakikisha wanakuwa na uwezo na wanatambua wajibu wao na kuwa na uelewa madhubuti katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Kupitia mafunzo haya, kwa hawa ambao tumekubaliana kuendesha hili Shirika tujue majukumu yetu vizuri katika kuihudumia jamii kwa kufuata sheria na taratibu za nchi,"amesema Maingu.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Makongo Maingu amesema kuwa, Bodi ya Shirika hilo ina wajibu wa kufanya kazi kwa kuongoza shirika kufikia malengo yake ikiwemo kuweka vipaumbele na malengo ya shirika na miongozo ya kupata rasilimali za kuendesha shirika, na kupitia na kutathimini utekelezaji wa mipango ya shirika hilo.
Aidha, amewahimiza kusimamia uwajibika wa bodi na sekretarieti kwa kuweka sera, miongozo na kanuni mbalimbali, kuhakikisha mikataba yote ya ubia inaendana na malengo na amali za shirika, kuhakikisha utekelezaji wa sheria na maagizo halali ya serikali na kusimamia matumizi ya rasilimali fedha.
Pia, amewaomba kusimamia na kutangaza heshima ya Shirika hilo ikiwemo ushiriki wa wajumbe wa bodi katika shughuli muhimu, kuimarisha Mawasiliano na watendaji, serikaki ngazi husika na jamii kwa ujumla pamoja na kuepuka maslahi mgangano.
Amewaasa pia, kuendeleza utamaduni wa kujifunza na kuelimishana kwa kushiriki kikamikifu katika fursa za mafunzo, kutoa taarifa za fursa na mafunzo zenye tija kwa Shirika pamoja na kujitolea kufundisha na kuwezesha wajumbe wa bodi na wadau wengine.

Pia, kufanya usimamizi madhubuti wa rasilimali na fedha kwa kutathmini ubora wa kubuni na kupendekeza mabadiliko na kuandaa taarifa za fedha, kusimamia uandaaji wa bajeti ya mwaka na usimamizi wa shughuli za kila siku za shirika.
Kwa upande wake, Tendo Makori ambaye ni Mjumbe wa Bodi aliyeshiriki mafunzo hayo amesema, mafunzo hayo yatamsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake na yamemsaidia kumuongezea ufanisi.