NA FRESHA KINASA
OFISI ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara chini ya Mbunge Prof. Sospeter Muhongo imebainisha kuwa,kuna mambo kadhaa ambayo yalichangia matokeo ya kutoridhisha ya miaka mitatu mfululizo (2020, 2021 na 2022) kuanzia kidato cha pili na nne jimboni humo.
Picha zikiwaonesha walimu wakuu wa shule za sekondari za Musoma Vijijini wakiwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo kwenye kikao chao cha Februari 3, 2023 kilichofanyika Busambara Sekondari iliyopo Kijiji cha Kwikuba.
Hayo yamebainishwa kupitia sehemu ya pili ya taarifa ya kikao cha Mbunge wa jimbo hilo na wakuu wa shule za Musoma Vijijini iliyotolewa na ofisi hiyo leo Februari 20, 2023.
Vikao hivyo vya tathimini ya kina kwa nyakati tofauti viliangazia mambo mbalimbali ya msingi ikiwemo kwa nini ufaulu siyo mzuri kwenye sekondari za Musoma Vijijini? Nini kifanyike kuongeza uelewa na ufaulu kwa wanaojifunza (wanafunzi).
Pia nini kifanyike kuongeza umahiri na uwajibikaji wa kufundisha kwa walimu wetu? Na majukumu ya wazazi ni yapi?.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini imefafanua kuwa, matokeo ya kutoridhisha ya mwaka 2022 kulingana na tathimini ya vikao hivyo ilielezwa kuwa, yalichangiwa na kubadilika kwa mfumo wa utungaji wa mitihani unaozingatia umahiri, yaani, "competence based" badala ya ule mfumo uliozoeleka wa kukariri. Matayarisho ya mabadiliko hayo hayakuwepo.
Aidha,matokeo ya kutoridhisha ya miaka mitatu mfululizo (2020, 2021 na 2022) imetajwa chanzo ni pamoja na wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda masomoni. Wapo wanaotembea zaidi ya kilomita tano kwenda masomoni.
Pia wanafunzi kukosa chakula wawapo masomoni (kifungua kinywa na chakula cha mchana) na wapo wanafunzi waliopanga vyumba kwenye vijiji vya karibu na sekondari wanazosoma. Hawa wanafunzi wapangaji wanaishi kwa kujitegemea kama ziishivyo kaya zetu.
Wakati huo huo, taarifa hiyo imefafanua kuwa, sababu nyingine ni sekondari nyingi hazina maabara na vifaa vyake kwa masomo ya sayansi (chemistry, physics and biology laboratories).
"Sekondari karibu zote hazina maktaba. Vitabu vya maktaba vipo vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo, changamoto nyingine ni uhaba wa vitabu vya kiada ambapo uwiano unapaswa kuwa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. Uwiano huo kwa sasa, kwa baadhi ya sekondari, ni kitabu kimoja kwa wanafunzi watano,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, imebainika kuwa,lugha ya kufundishia ya Kiingereza bado ni tatizo. "Hata lugha yetu ya Taifa (Kiswahili) bado uelewa na ufaulu wake hauridhishi,"imeongeza taarifa hiyo.
Walimu
Katika hatua nyingine, imebainika kuwa, upungufu mkubwa wa walimu ambao hauendani na uwiano wa walimu na wanafunzi (ratio: teacher/students) ni changamoto. Kwa mfano ipo Sekondari ina wanafunzi 1,012 na walimu 13 tu. Pia ipo sekondari mpya yenye wanafunzi 158 na walimu watano tu.
"Uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi. Kwa mfano, kuna Sekondari zenye mwalimu mmoja tu wa Hisabati na mmoja tu wa Fizikia kwa madarasa yote, kidato cha kwanzia hadi cha nne,"imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, upungufu na uhaba mkubwa wa walimu unalazimisha sekondari kuajiri walimu wa kujitolea ambao wanalipwa posho na wazazi, na Mbunge wa Jimbo huwa anachangia kwa baadhi ya sekondari.
Sambamba na kuweka wanafunzi kati ya 50 na 60, au zaidi ndani ya chumba kimoja cha darasa ili kupunguza mizigo ya vipindi vyingi kwa baadhi ya walimu.
Hata hivyo, kutokana na changamoto hizo, ili kufikia lengo mapendekezo ya kuongeza ubora wa kujifunza na kufundisha kwenye shule Musoma Vijijini yametolewa.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kutokana na mapungufu na mahitaji yaliyoelezwa hapo juu, kwa upande wa wanafunzi na walimu, yanapaswa yatatuliwe kwa ushirikiano wa wahusika wote.
Pia, wazazi wametakiwa watimize wajibu wao wa malezi mazuri ya watoto wao, na wafuatilie kwa karibu sana mienendo na tabia za watoto wao, kama vile kushinda kwenye runinga (TV), kubeti, kamari na kucheza pool.
"Wazazi watimize wajibu wao wa kuwanunulia watoto wao mahitaji ya shule na elimu kwa ujumla.Wazazi wakubali kuchangia chakula cha mchana cha watoto wao wawapo masomoni na azazi waache kuwapa watoto wao kazi za kiuchumi za familia wawapo masomoni, kwa mfano, kuwatuma kuchunga mifugo, kuvua samaki, kuchimba madini, na kuuza bidhaa sokoni wakati wa vipindi masomoni,"imesisitiza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, imebainisha kuwa, Sera ya Elimu Bila Malipo iendelee kufanunuliwa na wahusika ili wazazi wasiache kutimiza wajibu wao wa kuchangia upatikanaji wa elimu nzuri kwa watoto wao.
Aidha, wazazi na walimu waendelee kuboresha uhusiano kati yao kwa manufaa ya uboreshaji wa elimu itolewayo kwenye shule zao.
"Walimu waongezewe mafunzo wawapo kazini. Mafunzo yatolewe mara kwa mara ndani ya kipindi kifupi cha miaka 2-3.Kuwepo msawazo sawa kwa wingi (fair distribution) wa walimu kwenye sekondari za vijijini na mijini ndani ya halmashauri, wilaya na mkoa.
"Vile vile, maslahi ya walimu yaboreshwe kwa kiwango kikubwa, yaani walimu wajengewe nyumba za kuishi hasa wale wanaofundisha vijijini, mishahara ya walimu iboreshwe sana na makato yake yapunguzwe.
"Nchi ambazo zinaongoza Dunia kwa ubora wa elimu, mishahara ya walimu wao iko juu kuzidi taaluma nyingi nchini humo. Kitengo cha uthibiti ubora kiongezewe uwezo wa kufuatilia shughuli za ufundishaji na ujifunzaji mashuleni,"imefafanua sehemu ya taarifa
Mbali na hayo imetakiwa kuimarisha lugha za kufundishia na kujifunzia kwa shule za msingi na sekondari ikiwemo kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri kwenye mitihani inayotolewa.
"Waliopewa majukumu ya kiuongozi ya kusimamia masuala ya elimu kwenye shule wawe na uwezo wa kielimu wa kutekeleza majukumu yao,"imebainisha taarifa hiyo.