NA OR-TAMISEMI
WAGANGA wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini wamehimizwa kufanya usimamizi wa afya shirikishi (Cascade Supervision) kwa zahanati zinazowazunguka ili kuziongezea nguvu zahanati hizo katika kuboresha huduma za afya, pamoja na kupunguza rufaa za wagonjwa katika ngazi vituo vya afya na hospitali za halmashauri.
Rai hiyo imetolewa Februari 3, 2023 na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OR-TAMISEMI), Dkt.Ntuli Kapologwe wakati wa kikao kazi cha timu ya usimamizi shirikishi kutoka Idara ya Huduma za Afya OR-TAMISEMI na timu za uendeshaji wa huduma za afya Mkoa wa Mtwara.
"Lengo la Cascade Supervision ni kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika zahanati na kupunguza wagonjwa wanaotoka katika zahanati na kwenda katika vituo vya afya kupata huduma ambazo wamezikosa,"amesema Kapologwe.
Sambamba na hilo amewahimiza viongozi hao kutoa huduma za mkoba (Outreach Services) katika maeneo yao ili kuwahudumia wananchi ambao wapo mbali na vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Majengo, Dkt,Mohmoud Mohmoud amethibitisha kuwa usimamizi shirikishi kwa zahanati unaimarisha na kuboresha utolewaji wa huduma za afya msingi kwa kuwa Kituo cha Afya Majengo ni mojawapo ya kituo kinachofanya zoezi hilo.
"Katika kituo chetu cha afya Majengo tulifanya usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za clinic ya uzazi kwa zahanati zinazotuzunguka,hii imesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuimarisha huduma za afya pamoja na kuongeza mapato ya zahanati zinazotuzunguka,"amesema Mahmoud.