Walimu Kasulu watakiwa kutekeleza vigezo 19 vya kupima utendaji kazi

NA RESPICE SWETU

KUWEKWA kwa vigezo 19 vya kupima utendaji kazi wa walimu wa shule za msingi nchini, idara ya elimu awali na msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imewataka walimu kutekeleza vigezo hivyo.
Maagizo hayo yametolewa kwa nyakati tofauti na maafisa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu walipokutana na walimu wa halmashauri hiyo pamoja na wadau mbalimbali kuweka mikakati ya kutekeleza vigezo hivyo.

Wamesema kuwa, utekelezaji wa vigezo hivyo ni muhimu kwa kuwa utasaidia kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kitaifa na kwenye halmashauri yetu ambayo haikufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa upimaji darasa la nne na mtihani wa kuhitimu darasa la saba iliyofanyika mwaka jana.

Akitoa taarifa ya matokeo ya mitihani hiyo, afisaelimu taaluma wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Joseph Maiga alisema halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imekuwa ya tano kati ya halmashauri nane za mkoa wa Kigoma kwenye mtihani wa kuhitimu darasa la saba na ya saba katika mtihani wa upimaji wa darasa la nne.

"Matokeo hayo sio mazuri kwetu na hata kitaifa na kutokana na sababu hiyo, Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya elimu wamefanya tathmini wakaja na vigezo 19 vya upimaji vitakavyosaidia kupandisha ufaulu huo,"amesema.

Akivitaja vigezo hivyo Maiga alisema kuwa, miongoni mwa vigezo vilivyopo ni kwa kila shule kufanya tathmini pindi matokeo ya mitihani yanapotoka, kudhibiti utoro na kukabiliana na mdondoko wa wanafunzi.

Alieleza pia kuwa kigezo kingine ni walimu kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba kwa asilimia 95 huku wanafunzi wa darasa la nne wakitakiwa kuwa na ufaulu wa asilimia 100.
Aidha, vigezo hivyo vinaitaka kila shule kuweka mkakati wa kuhakikisha watoto wa darasa la kwanza wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Vigezo hivyo vitakavyotumika nchi nzima, vinawataka pia walimu kuwawezesha wanafunzi wa darasa la tatu kumudu stadi za somo la kiingereza.

Akifafanua kuhusu stadi hizo Maiga alizitaja kuwa ni za kuzungumza, kusikiliza, kuandika na kusoma.

Vigezo hivyo vimewataka pia walimu kushirikiana na kamati za shule, wazazi na jamii ili kuwezesha upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni.

Akizungumza na walimu wa kata ya Nyamidaho katika kikao kilichofanyika kwenye shule ya Msingi Mvugwe, afisaelimu wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Elestina Chanafi alisema ni jukumu la kila mmoja kutekeleza vigezo hivyo.

"Baada ya kuwasilisha vigezo hivi tutaanza kupita ili kuona utekelezaji wake, tumepewa siku mbili tu za kukaa ofisini na siku zinazobaki tutakuwa shuleni", amesema.

Amewataka walimu kufanya kazi kwa kujituma na kuifanya kazi hiyo kuwa ndio kipaumbele chao.

"Mnatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuacha alama katika shule zenu, msichanganye muda wa kazi na mambo mengine na anayeona biashara inalipa kuliko kazi aache kazi", amesema.

Katika kikao hicho Chanafi alirudia kauli aliyowahi kuitoa hivi karibuni kuwa "mwaka huu afe kipa afe beki" akiashiria dhamira ya kusimamia utekelezaji wa vigezo hivyo na kuinua taaluma, kauli hiyo aliitoa mara ya kwanza alipokuwa akizungumza na walimu wa kata ya Buhoro.
Kikao hicho kilihitimisha mzunguko wa maafisa elimu kukutana na walimu pamoja na wadau wengine ambapo takriban walimu 800 wamefikiwa sambamba na watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, wenyeviti wa kamati za shule,madiwani pamoja na viongozi wa madhehebu ya dini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news