WANACHAMA WA CHF WATAKAVYONUFAIKA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE

NA MWANDISHI WETU

MPANGO wa Bima ya Afya kwa Wote, ni moja ya mpango madhubuti ambao umelenga kuhakikisha kila mwananchi wa Tanzania ananufaika kwa kupata huduma za matibabu bila ya kikwazo chochote cha fedha.
Kumekuwa na kilio cha miaka mingi kwa wananchi juu ya upatikanaji wa huduma za matibabu ambapo wachache ndio walikuwa na uhakika wa kuzipata huduma hizo hususani watumishi wa umma ambao walijiunga kupitia NHIF.

Kundi kubwa la wananchi lilikuwa nje ya mfumo wa bima ya afya na wengine wakiwa kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao nao huduma zake hazikuwa na wigo mkubwa kwa maana ya vituo vya huduma pamoja na wigo wa huduma za matibabu.

Kukosekana kwa Mfumo mzuri wa kupata huduma za matibabu ndiko kulipelekea Serikali kuanza mchakato wa Bima ya Afya kwa wote na suala hili kuwekewa msisitizo mkubwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amesikika mara kadhaa akielekeza wataalam kukamilisha mchakato huo.

Habari njema ni kwamba kesho Alhamisi tarehe 9 Februari, 2023 Bunge litajadili Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote na endapo utaridhiwa Julai Mosi, 2023 sheria hiyo itaanza kutumika rasmi.

Muswada huu unazo faida nyingi kwa wananchi wote lakini pia kwa wanachama waliokuwa kwenye CHF ambao awali hawakupata huduma nyingi hususan za kibingwa ambazo walilazimika kuwa na fedha ili wapate huduma hizo hivyo ilikuwa ni changamoto kubwa kwao na mfano wa huduma hizo ni pamoja na vipimo vikubwa kama CT-SCAN, MRI na vingine lakini huduma za magonjwa makubwa kama saratani, moyo na mengine.

Bima ya Afya kwa wote inaleta usawa kwa wananchi katika kupata huduma na watapata huduma hizo kuanzia ngazi ya zahanati hadi ngazi ya Taifa jambo ambalo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi na kuwaepushia kuingia kwenye umasikini wa kuuza mali za familia ili kugharamia huduma za matibabu.

Ufinyu wa huduma za CHF ziliwafanya wananchi kushindwa kupata huduma nje ya kituo alichojiandikisha na hivyo kulazimika kulipia gharama za matibabu na hii iliondoa maana nzima ya kuwa na bima ya afya.

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote una lengo la kutatua changamoto hizo kwa kuanzisha Kitita cha Mafao ya huduma za Msingi cha Jamii ambacho kimelenga wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi ikijumuisha wanachama waliokuwa wanufaika wa Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa.

Kitita hicho kitaanzishwa ndani ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo usimamizi na uendeshaji wake utakuwa kama ilivyo kwa vitita vya mafao vinavyotolewa na Mfuko kwa sasa hivyo mwanachama kuwa na uhakika zaidi wa kupata huduma kwa kuwa NHIF tayari ina wigo mpana wa Vituo.

Aidha, ili kukidhi utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Mfuko umewekeza zaidi katika kuimarisha mifumo ya TEHAMA badala ya kuajiri watumishi wengine, hivyo haitarajiwi kuongeza gharama za uendeshaji wa Mfuko.

Kutokana na haya ni wakati sasa Watanzania kwa pamoja tuunge mkono jambo hili kubwa ili kila mwanachi awe na uhakika wa huduma za matibabu wakati wowote anapozihitaji bila ya kikwazo chochote.

BIMA YA AFYA TANZANIA INAWEKEZAKANA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news