NA MWANDISHI WETU
WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wanatarajiwa kumegewa eneo lenye ukubwa wa hekta 10,828 kutoka katika Msitu wa Hifadhi wa Loasi kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja kwa Niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Mhe.Aida Khenani kuhusu mkakati wa Serikali wa kuwapatia wananchi maeneo ya kulima kutoka kwenye mapori na hifadhi ambazo hazina wanyamapori.
Amesema, kufuatia uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta, Wilaya ya Nkasi inapaswa kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya wananchi kwa kuwa wilaya hiyo haina uhaba wa maeneo bali inakabiliwa na changamoto ya mgawanyo na mtawanyiko wa makazi na shughuli za kibinadamu.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhe. Mary Masanja amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi na kujichukulia sheria mkononi kwa kuwadhuru wahifadhi wanaolinda rasilimali za Taifa.
“Tunasikitishwa sana na vitendo vya wananchi wanaojichukulia sheria mkononi na kudhuru askari wetu wa uhifadhi. Askari hawa wanalinda rasilimali hizo kwa niaba ya Watanzania, tunaomba wananchi washiriki kuyalinda maeneo haya wasijichukulie sheria mkonon,"amesisitiza Mhe. Masanja.