WAZIRI DKT.BITEKO AZINDUA KAMATI MPYA YA TEITI

*Aitaka kuleta matokeo chanya katika usimamizi wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko amezindua Kamati ya tano ya Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) inayosimamia viwango vya uwazi na uwajibikaji kwa lengo la kuboresha mapato na manufaa yatokanayo na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini.
Dkt. Biteko amezindua kamati hiyo leo Februari 9, 2023 katika ukumbi wa Abdulkarim Mruma uliopo jijini Dodoma itakayofanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2023 mpaka 2026.

Sambamba na uzinduzi huo, Dkt. Biteko amewakabidhi wajumbe wakamati hiyo vitendea kazi vitakavyo tumika katika kutekeleza majukumu yao ambavyo ni Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia na Kanuni zake, Sheria ya Madini , Sheria ya Petroli, Sheria ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi pamoja na EITI Standard 2019.
Akizungumza juu ya majukumu ya kamati hiyo, Dkt. Biteko amesema kuwa, katika kutekeleza majukumu hayo wajumbe wa kamati hiyo wanatakiwa kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitawezesha kuchangia ukuaji wa sekta ya Uziduaji hapa nchini kwa kuzingatia taarifa za malipo na mapato za wachimbaji wadogo wa madini zinawekwa wazi na kulinganishwa.

Akielezea juu ya madini mkakati,Dkt. Biteko amesisitiza kuwa kwa sasa dunia inasisitiza utafutaji na uchimbaji endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira hivyo ameitaka kamati kuisimamia Taasisi hiyo katika tafiti mbalimbali zitakazowezesha serikali na wadau wa maendele kuwekeza katika madini hayo muhimu duniani.
Akifafanua kuhusu mhamo wa nishati, ameitaka kamati kuweka nguvu katika kuhamasisha uwazi na kutoa elimu kuhusu mhamo wa nishati kwa kushirikiana na taasisi zingine za Serikali katika kuandaa mpango wa kutambua madini mkakati na kuishauri Serikali juu ya maendeleo endelevu ya Sekta ya Uziduaji nchini.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kamati ya TEITI,Ludovick Utouh amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali zinazosimamiwa na TEITI ambayo ilijiunga na Asasi ya EITI Mwezi Februari 2009 ili kuhakikisha kuwa inaweka mifumo ya Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa lengo la kuboresha mapato na manufaa yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini.
Sambamba na malengo hayo, Utouh amefafanua kuwa, TEITI itaendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini kwa lengo la kufikia kiwango cha mchango wa asilimia 10 katika la Pato la Taifa ifikapo 2025 kulingana na Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano.
Uzinduzi wa kamati ya tano ya TEITI umeudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Danstan Kitandula, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news