NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu na timu yake kwa kuendelea kuwa wabunifu ili kuhakikisha shirika linazidi kuimarika na kutekeleza miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi na Taifa.
Mheshimiwa Dkt.Mabula ametoa pongezi hizo leo Februari 17, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini Hati ya Maelewano (MoU) baina ya Benki ya Absa Tanzania na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa lengo la benki hiyo kuwezesha wateja wake kupata mkopo ulioboreshwa kwa ajili ya manunuzi ya nyumba.
"Na mimi kwa bahati mbaya sio Marketing Officer (afisa masoko) wala sifahamu kuhusu marketing (masoko), lakini Nehemia ameifanya kazi hii vizuri sana, niwapongeze sana kwa namna ambavyo mnafanya kazi yenu.
"Nitafurahi kusikia baada ya kuwa mmeshafanya saini yenu na mambo mengine basi walau hawa waliokuja mmepata walau wateja wasiopungua 10 ili waweze kutoka na kitu ambacho tunakitarajia hapa na nitangaze rasmi kwamba mkopo wa nyumba wa Absa ulioboreshwa na makubaliano ya mauzo ya awali ya nyumba kati ya Benki ya Absa Tanzania na Shirika la Nyumba la Taifa sasa imezinduliwa rasmi,"amefafanua Waziri Dkt.Mabula.
Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.45 ya mwaka 1962.NHC baadae liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 1990 ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.
Malengo ya shirika kwa mujibu wa Mpango Mkakati wake (2015/16-2024/25) ni pamoja na kuwa msimamizi mahiri wa miliki, kuimarisha uwezo wa kiuendeshaji na udhibiti, kutumia kikamilifu rasilimali watu, kuwa kiongozi katika uendelezaji miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika nchini.
Chini ya uongozi wa Mchechu, NHC limejiwekea maadili ya msingi sita ambayo ni weledi, ufanisi, uwazi, ubunifu, ushirikiano na uadilifu ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya kwa haraka.
Aidha, Waziri Dkt.Mabula amefafanua kuwa, nyumba ni hitaji muhimu kwa binadamu yeyote. "Sote tunatambua nyumba ni muhimu na ni hitaji la kila Mtanzania na kila mwanadamu. Kama ambavyo ilivyo katika Katiba yetu Ibara ya 24 ambavyo inazungumzia haki hii sambamba na haki za kupata chakula na mavazi.
"Haki ya kuwa na nyumba imewekwa kama kigezo kikuu cha kukuza uchumi na kudumisha amani duniani kote, kwa hiyo kilichofanyika hapa ni kwamba wanaendelea kutekeleza matakwa ya Katiba ya nchi yetu, vile vile uwekezaji katika Sekta ya Nyumba inachangia pia katika ukuaji wa mitaji, ajira kipato akiba na kuimarisha afya na elimu kama ambavyo sote tunafahamu.
"Serikali zote duniani zinathamini malengo ya Sekta ya Nyumba katika kukuza uchumi wa nchi na ni kichocheo cha kudumisha amani pia kama huna nyumba maana yake huna mahali salama pa kulala na hivyo huwezi kuwa na amani,"amefafanua Waziri Dkt.Mabula.
Amefafanua kuwa,pale unapokuwa na nyumba utakwenda kupumzika baada ya shughuli zako na amani itakuwepo. "Hivyo, hakuna nchi inayoendelea bila kutoa kipaumbele kwenye Sekta ya Nyumba, ninawapongeza kwa namna ambavyo mmekuja na products ambazo zinagusa maisha ya Watanzania,"amebainisha.