NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt .Angeline Mabula amezindua Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039.
Uzinduzi wa mpango huo umefanyika Februari 21, 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya, madiwani, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa taasisi za serikali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Dkt. Mabula alisema lengo kuu la kuandaa mpango kabambe wa Jiji la Mbeya ni kutoa dira ya namna jiji la Mbeya litakavyopaswa kukua na kuendelezwa kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia 2019-2039.
Mpango Kabambe uliozinduliwa umetaja mikakati minne ya kusimamia ukuaji na maendelezo ya Jiji la Mbeya ambayo ni uendelezaji upya maeneo kongwe, kurasimisha makazi ambayo kimipangomiji hayajaathirika sana, lakini kuna uwezekano wa kupata miundombinu, kusimamia yasiyoathirika kwa kuvamiwa na ujenzi holela pamoja na mkakati wa kuanzisha miji ya pembezoni.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akiwasili viwanja vya Kabwe mkoani Mbeya kwa ajili ya kuzindua Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na kushoto ni Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa.
Dkt.Mabula ametoa wito kwa taasisi zinazotoa huduma mbalimbali kwenye Jiji la Mbeya kuutumia Mpango Kabambe ulioandaliwa katika utekelezaji wa shughuli zao na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kuunda timu maalum itakayosimamia utekelezaji Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya na wajumbe wake watoke katika taasisi zote zinazowajibika kutekeleza miradi mbalimbali iliyoanishwa katika mpango huo.
Alisema, katika Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, uwekezaji katika viwanda na ujenzi wa miundombinu unatiliwa mkazo na msukumo mkubwa hivyo utayarishaji wa mpango kabambe ni hatua muhimu sana kufikia azma hiyo.
Aliongeza kwa kusema katika kufikia azma hiyo Wizara ya Ardhi imekuwa ikisisitiza kila mamlaka ya upangaji kuandaa mpango kabambe wa eneo lake ili kuendana na kasi ya utekelezaji wa azma hiyo na kuvutia wawekezaji.
Kwa mujibu wa Dkt.Mabula kwa kushirikiana na na mamlaka za upangaji jumla ya mipango kabambe 26 imekwisha idhinishwa na Wizara ya Ardhi ambapo kati ya hiyo sita ni ya majiji ikiwemo Jiji la Mbeya, 13 katika manispaa nasaba7 katika halmashauri za miji.
Ametoa rai kwa mamlaka za upangaji nchini kuandaa mipango kabambe ya maeneo yao kwa kutumia wataalamu washauri au wataalamu wa ndani kadri ya uwezo wa mamlaka ya upangaji.