NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji utakaogharimu takribani shilingi bilioni 120 unaotekelezwa katika vijiji 55 vya wilaya za Ruangwa (vijiji 34) na Nachingwea (vijiji 21) mkoani Lindi.
Amesema mradi huo ambao utatekelezwa na wakandarasi wawili wazawa ambao ni STC Construction Company Limited na Emirate Builders Co. Limited unatarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika wilaya hizo.
Waziri Mkuu ameshuhudia utiaji saini wa mkataba huo katika hafla iliyofanyika leo Februari 18,2023 kwenye ukumbi wa chuo cha VETA kilichopo Nandagala wilayani Ruangwa. Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakandarasi hao wakamilishe mradi huo kwa wakati.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi mingi ikiwemo ya maji ambayo ni ahadi ya Rais ya kumtua mama ndoo kichwani.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 ambayo inaielekeza Serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini unafikia zaidi ya asilimia 85 na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini ifikapo Mwaka 2025.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi ametoa wito kwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huo wahakikishe wanautekeleza kwa wakati na kwa uaminifu wa hali ya juu na kwamba wizara itawasimamia kwa ukaribu.
Naibu Waziri huyo amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani inatimia.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo amesema upatikanaji wa maji Ruangwa kwa sasa ni asilimia 68.2 na Nachingwea ni asilimia 67, hivyo kukamilika kwa mradi huo ambao utanufaisha wakazi zaidi ya 130,000 kutawezesha watu wengi zaidi kufikiwa na huduma hiyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia anazozifanya katika kuwaletea wananchi maendeleo, ambapo katika kipindi cha miaka miwili zaidi ya shilingi bilioni 300 zimepokelewa mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ikiwemo ya elimu na afya.