Askofu Dkt.Maboya:Popote penye mchele pana chuya,Dkt.Nabiijoshua songeni mbele

NA DIRAMAKINI

MLEZI wa Mitume na Manabii Tanzania, Askofu Dkt.Dustan Haule Maboya amesema Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT), Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ndiye alichaguliwa na kupitishwa kwa kauli moja kuwa rais wa umoja huo nchini.
Ameyasema hayo hivi karibuni katika maombi maalumu ya kuombea nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) katika Huduma ya PMIC City of Wonders Kilimanjaro iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro chini ya Nabii Esther Bukuku.

"Na ninamshukuru Mungu kwa ajili ya mtumishi wetu, Joshua Mwantyala yeye tulimchagua sisi kwa kura zote Anatogulo, na uchaguzi ule kulikuwa kuna Meya,kulikuwa kuna viongozi wote, Bishop Ndalima alisimamia hayo yote. 
"Bishop Mwasota alikuwepo, na sote tulimpitisha kwa kauli moja (Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala), tulimpitisha yeye, tukampitisha pamoja na mtumishi wa Mungu, Joshua Kalebu ndiyo walipita katika ule uchaguzi...

"Uchaguzi ulikwenda vizuri, lakini popote penye mchele pana chuya, chuya imekuwa ikijisogeza yenyewe kwa yenyewe, tuliongea na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati huo, Mheshimiwa Gorge Simbachawene. Alitupa jukumu moja la kuwaunganisha mitume na manabii nchi nzima. 

"Ili tuwe kitu kimoja, tuweze kutambulika serikalini, hiyo ndiyo ilituongoza tukafanya kampeni zote hadi hapa tulipofikia. Ninajua, hapa juzi kati, pametokea hitilafu kidogo, ya baadhi ya watu walioteuliwa, lakini si wale ambao waliochaguliwa Anatogulo, naomba utuelewe hivyo, nafasi nyingine zote hizi ambazo zilikuwa zimetokea za wajumbe wengine sizo zilizochaguliwa Anatogulo.

"Anatogulo tulimchagua Rais (Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala) na Katibu Mkuu (Joshua Kalebu) na viongozi wengine, na kuna watu walikuwa wanasema, itakuwaje mtu atokee Morogoro, nikawaambia sauti ya mtu iliyayo nyikani. 

"Sifa kubwa ya kiongozi ni kukubali kuongozwa, sema anayetaka kuwa mkubwa kwenu na awe mdogo. Sasa tumekwenda vile na tumefika eneo na ukweli,Rais wetu amejitahidi kwa njia nyingi sana,ingawa kuna baadhi ya watu ambao walikuwa wameteuliwa au tuliwateua kwenye nafasi zao, hawakuridhika kwa jambo moja au lingine, wakaamua kutoka.
"Ule ni uhuru wa mtu ambao alikuwa nao na wala ule si ugomvi, kumbuka Paulo hawakuelewana na Barnaba, kwa sababu Paulo alimpenda Sila kwa sababu alimchukuia Marko kwa sababu mvivu,lakini Barnaba alimlea Marko, baadae Paulo alikiri Marko amenisaidia, hauwezi ukajua haya yanayotokea leo, kesho na kesho kutwa hawa watu wakarudi kuwa kitu kimoja,"alifafanua Dkt.Maboya.

Rejea katika Biblia Takatifu,Matendo ya Mitume 15:36-18:22..."Baada ya siku chache Paulo alimwambia Barnaba, “Twende tukawatembelee ndugu katika miji yote ambamo tulihubiri neno la Bwana tuone jinsi waamini wanavyoendelea.” 37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana Marko waende naye. 

38 Lakini Paulo aliona si vizuri kumchukua kwa sababu aliwahi kuwakimbia walipokuwa huko Pamfilia, akakataa kuendelea kufanya kazi nao. 

39 Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba juu ya jambo hili, wakatengana. Barnaba akamchukua Yohana Marko akaenda naye Kipro. 40 Paulo akamchagua Sila akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana. 41 Naye akapitia Siria na Kilikia wakaimarisha makanisa ya huko..." 

Hivi karibuni,Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania alitwaa asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa nafasi ya urais katika Umoja wa Manabii na Mitume nchini Tanzania (Unity of Apostles and Prophets Tanzania).

Ushindi huo ulitokana na kura 179 alizopata huku akiwaacha mbali washindani wake akiwemo Mchungaji Ceasar Masisi aliyepata kura 42 na Mtume Joackim Kimanza aliyepata kura nne kupitia uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Anatoglo uliopo Ilala, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Askofu Profesa Rejoice Ndalima alimtangaza rasmi Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala kuwa Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii nchini Tanzania.

Aidha, mitume na manabii mbalimbali nchini walionesha imani kubwa juu ya Dkt.Nabiijoshua huku wakimpongeza na kuahidi kumpa ushirikiano mkubwa aweze kutekeleza jukumu lake la kuwaunganisha viongozi hao wa kiroho ili waweze kulihubiri neno la Mungu kwa ufanisi nchini.

Wakati huo huo,Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania (UMMT) siku ya Aprili Mosi, mwaka huu itakuwa ndiyo Siku ya Kitaifa ya Kongamano la Mashangilio litakalofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Ubungo Plaza panatajwa kuwa ni mahali pazuri sana kusherehekea hafla nyakati zote kwa sababu iko katikati ya jiji, na mawasiliano mazuri, maegesho, lifti na huduma zingine ambazo husaidia kuwezesha kila kitu unachohitaji kufurahia wakati wako.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news