BINTI:MSIMAMO TAMBO YAKO-7

NA LWAGA MWAMBANDE

UTENZI huu ni sehemu ya Mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana (0752 352 116) wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo ameyatoa katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya mabinti.

Hii ni sehemu ya saba na ya mwisho ya utenzi huu. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, Mungu ambariki Pastor Katana kwa elimu hii nzuri kwa walengwa na awabariki wote ambao mtaendelea kufuatilia na kufaidika na mafundisho haya. Endelea;

1. Msimamo tambo yako,
Katika maisha yako,
Ndiyo upekee wako,
Na pia thamani yako.

2. Mambo mengimengi yako,
Wanayopenda wenzako,
Kitaka kuvuta huko,
Chunga msimamo wako.

3. Siyo yote mambo huko,
Hayaendani na yako,
Lakini siende huko,
Ichunge mipango yako.

4. Wapo watu wengi huko,
Wanafanya yao huko,
Wakiupata mwaliko,
Nao wanakwenda huko.

5. Maendeleo hayako,
Bendera upepo huko,
Yao yanafia huko,
Chunga msimamo wako.

6. Unayo ratiba yako,
Ya kufanya mambo yako,
Akija yeyote kwako,
Shika msimamo wako.

7. Usiache kazi zako,
Kwa sababu ya mwenzako,
Na ajenda mpya kwako,
Ni uangamivu wako.

8. Umeumbwa peke yako,
Unayo maisha yako,
Wanaoburuza wako,
Shika msimamo wako.

9. Wamwamini Mungu wako,
Sawa na kitabu chako,
Kuyumba hatari kwako,
Chunga msimamo wako.

10. Si kwamba mengine huko,
Kwamba hayafai kwako,
Ni uangalifu wako,
Usiache njia yako.

11. Bila msimamo wako,
Utafanya ya wenzako,
Ukijibomoa kwako,
Chunga msimamo wako.

12. Huo msimamo wako,
Ulete heshima kwako,
Hata kwa hao wenzako,
Chunga msimamo wako,

13. Wasema bidada yuko,
Hataki ujinga huko,
Sipeleke yako huko,
Huo msimamo wako.

14. Ukisimamia yako,
Hiyo ni heshima kwako,
Na tena busara yako,
Chunga msimamo wako.

15. Fanya watu waje kwako,
Wape maujuzi yako,
Waige mwenendo wako,
Chunga msimamo wako.

16. Kwa kutokuyumba kwako,
Utafanya mambo yako,
Mungu kiongozi wako,
Chunga msimamo wako.

17. Ni vipi nafasi yako,
Katika maisha yako,
Kuna msimamo huko?
Chunga msimamo wako.

18. Tawala maisha yako,
Uyapange mambo yako,
Kiongozi Mungu wako,
Huo msimamo wako.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news