BINTI:MWENDO WAKO NURU YAKO-5

NA LWAGA MWAMBANDE

BINTI, fahamu kuwa, kila binadamu ana mfumo wa maisha yake,hivyo ili uweze kusonga mbele angalia maisha yako na msikilize Mungu anasema nini juu yako na siyo mwanadamu anasema nini.

Picha na Freepik

Zingatia,ukisilikiliza ya mwanadamu maisha yako yatakuwa ya ugomvi kila uchwao, lakini ukimtegemea Mungu, kwa neema ya Yesu Kristo hakuna jambo gumu katika mipango na safari yako ya maisha. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakuambia kuwa,mwendo wako ndiyo nuru wako. Endelea;

1. Vipi wewe watembea,
Mbona kama wazembea,
Unategeategea?
Mwendo wako nuru yako.

2. Kuna siri kutembea,
Binti nakuelezea,
Urembo kwaelezea,
Mwendo wako nuru yako.

3. Vile unavyotembea,
Tausi wapendezea,
Twiga wajielezea,
Mwendo wako nuru yako.

4. Ni wa pekee tembea,
Nafasi wajiombea,
Waweze kukutokea,
Mwendo wako nuru yako.

5. Binti maringo tembea,
Na sifa hizo pokea,
Mbele ukiendelea,
Mwendo wako nuru yako.

6. Nani unamtegea,
Na mbele waendelea,
Posa hujaipokea?
Mwendo wako nuru yako.

7. Napokwenda tembea,
Kukimbia wapotea,
Ni kama unazembea,
Mwendo wako nuru yako.

8. Kama mbali waendea,
Wahi huku watembea,
Ni ushauri pokea,
Mwendo wako nuru yako.

9. Kupuyanga wapotea,
Yashindwe kuwaelea,
Kule unakokwendea,
Mwendo wako nuru yako.

10. Asteste tembea,
Hatua twaelezea,
Watu watakuchekea,
Mwendo wako nuru yako.

11. Mchuchumio tembea,
Swaga zinazoenea,
Siyo kututelezea,
Mwendo wako nuru yako.

12. Na raba zako tembea,
Kama watutembelea,
Ndivyo unaendelea,
Mwendo wako nuru yako.

13. Na sendo zako chochea,
Kwa mwendo wajitetea,
Hata kujielezea,
Mwendo wako nuru yako.

14. Hujaolewa tembea,
Hujachumbiwa tembea,
Ndivyo wajielezea,
Mwendo wako nuru yako.

15. Wewe si sumu tembea,
Ndivyo unajitetea,
Na maji kujiombea,
Mwendo wako nuru yako.

16. Sirukeruke tembelea,
Na kwa kutulia tembea,
Njiani wewe enea,
Mwendo wako nuru yako.

17. Mwendo wakipendelea,
Moyoni ukaenea,
Mengine wataendea,
Mwendo wako nuru yako.

18. Salamu utapokea,
Mwendo kikuelezea,
Hata posa kupokea,
Mwendo wako nuru yako.

19. Wengi walioenea,
Kwao wanachekelea,
Ni jinsi wanatembea,
Mwendo wako nuru yako.

20. Kwani watu hutokea,
Kupenda yako tembea,
Mengine yaongezea,
Mwendo wako nuru yako.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Utenzi huu ni sehemu ya Mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana (0752 352 116) wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo ameyatoa katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya Mabinti. Mashairi yako katika sehemu saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news