BoT yaongeza muda wa usimamizi wa Yetu Microfinance Bank Plc

NA DIRAMAKINI

BENKI Kuu ya Tanzania imeongeza muda wa usimamizi wa Yetu Microfinance Bank Plc baada ya kuchukua uamuzi huo Desemba 12, 2022.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 14, 2023 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba.

"Itakumbukwa kwamba, kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha sheria namba 56(1)(g)(iii) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006,Benki Kuu ya Tanzania iliamua kuchukua usimamizi wa Yetu Microfinance Bank Plc kuanzia tarehe 12 Disemba 2022 baada ya kubaini kuwa ilikuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

"Baada ya kuchukua usimamizi wa benki hii, Benki Kuu ya Tanzania ilisitisha shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Yetu Microfinance Bank Plc kwa muda wa siku tisini ili kuipa nafasi Benki Kuu ya Tanzania kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili.

"Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuarifu umma kuwa mchakato wa kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya Yetu Microfinanc Bank Plc haujakamilika, hivyo muda wa usimamizi umeongezwa kwa kipindi cha siku thelathini kuanzia Machi 12,Machi 2023.

"Benki Kuu ya Tanzania inauhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha,"amefafanua Gavana Tutuba kupitia taarifa iliyotolewa leo.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news