CHOTORA:Jali usalama, Jali afya yako, Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa!!!

NA LWAGA MWAMBANDE

AGOSTI 26, 2022 Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati liliteketeza vipodozi na bidhaa za vyakula zilizoisha muda zaidi ya tani 31.2 zenye thamani ya shilingi milioni 100.9 katika Dampo la Chidaya jijini Dodoma.

Mkaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati, Domisiano Rutahala wakati akizungumza na waandishi wa habari katika dampo la Chidaya ambako ndiko bidhaa hizo na vipodozi viliteketezwa alisema,bidhaa na vipodozi zilizoteketezwa ni kutoka Dodoma,Singida na Tabora na ni kuanzia Novemba 2021 hadi Agosti 2022.

Aidha, mtaalamu huyo alisema bidhaa zilizoteketezwa ni zile zilioisha muda pamoja na vipodozi vyenye viambata vya sumu na vilivyoisha muda wake tani 31.2 sawa na kilo 3200.

TBS kupitia mtaalam huyo alisema wanateketeza bidhaa hizo kutokana na kuwa na madhara makubwa katika mwili wa mwanadamu ikiwemo kutopatikana kwa virutubisho vinavyohitajika na kusababisha magonjwa ya muda mrefu na mfupi kama saratani.

Kwa upande wa vipodozi, alisema vinaathari kubwa kiuchumi na madhara ya muda mfupi na mrefu ikiwemo kuathiri mifumo ya macho,ukuaji wa watoto na kina mama wajawazito.

Domisiano Rutahala aliwaasa wafanyabiashara wote kuwa makini kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa zao na wajiepushe na uuzaji wa bidhaa zenye viambata vya sumu kwani vina madhara makubwa na wazingatie maelekezo ya utunzaji wa bidhaa hizo ili kuendana na uzalisha pamoja na kulinda ubora wake. Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema, bidhaa zilizochotara hutupwa ili kulinda afya ya mtumiaji na kuepusha madhara mengine kiuchumi huku akisisitiza kuwa, kila mmoja yafaa kutumia bidhaa bora kwa ustawi bora wa afya na maisha. Endelea;


1.Bidhaa zikichotora, usiache zikakaa,
Japo kwa mtu hasara, kwa uhai inafaa,
Kutumia ni madhara, mwilini yaweza jaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

2.Bidhaa zilochotora, hizo haziwezi faa,
Kuzitupa jambo bora, kwa vile zimechakaa,
Kuziacha zinakera, zinaweza kuzagaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

3.Kwa tajiri na fukara, hizo haziwezi faa,
Tumia waweza hara, hata mwili kuchakaa,
Pia kupata hasara, kazi haiwezi faa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

4.Siyo jambo barabara, kuzificha zikakaa,
Tena kweli inakera, kuzifanya zinafaa,
Hata kama zinang’ara zimechotora kata,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

5.Kwa kweli ni jambo bora, umakini unafaa,
Bidhaa nazo chotora, kando ziweze kukaa,
Ni bora kuwa imara, tuziepuke hadaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

6.Kuna watu ni hasara, kotekote wazagaa,
Bidhaa zilochotora, hizo ndizo wazivaam
Wanatughilibu sura, watuuzia zakaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

7.Hao hasa ni wakora, wataka tukachakaa,
Kwani bidhaa chotora, kila kitu chachakaa,
Kitu ukione bora, chachakaa washangaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

8.Nondo zilizochotora, nyumba jenga yachakaa,
Waweza pata hasara, chini hiyo ikakaa,
Hakiki bidhaa bora, usijepata balaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

9.Vyakula viliwe bora, siyo vilivyochakaa,
Kula vilivyochotora, magonjwa wajiandaa,
Kansa matumbo safura, vyaweza kukuvagaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

10.Tumia bidhaa bora, na maisha yatapaa,
Lakini zilochotora, utazidi kuchakaa,
Hebu epuka hasara, kwa vitu bora komaa,
Zimeisha muda wake, kuzitupa inafaa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news