Deby ya Simba Queens, Yanga Princess kupigwa Uhuru leo

NA DIRAMAKINI

KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula amesema katika mchezo wa Derby wa leo dhidi ya Yanga Princess hakuna mchezaji yoyote ambaye watamkosa kwa sababu yoyote.

Lukula amesema, maandalizi yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kupambana kwa ajili ya kuhakikisha alama tatu zinapatikana hasa ukizingatia wataingia wakiwa wanaongoza ligi.

Amesema kuwa, siku zote mechi ya Derby inakuwa ngumu, lakini kwa upande wao hawataki kupoteza alama yoyote kwa sababu lengo lao ni kutetea ubingwa.

“Tunaenda kucheza mechi ya Derby tukiwa tunaongoza, hatutaki kupoteza alama yoyote kwa kuwa lengo letu ni kuchukua ubingwa ili tupate nafasi ya kushiriki CECAFA na baadae Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Kama tunataka kuchukua ubingwa tunapaswa kushinda mechi kama hii. Ligi ya msimu huu ni ngumu ndio maana hata ukiangalia msimamo tofauti ya pointi tumeachana alama chache,”amesema Lukula.

Kwa upande wake nahodha wa kikosi, Mwanahamisi Omary amesema wamepata maandalizi mazuri na wapo tayari kwenda kufanya kazi ambayo wanatakiwa kuifanya leo.

“Tumejiandaa vizuri kwa mchezo, hii ni Derby kubwa, sisi wachezaji tupo tayari kufanya kazi ambayo tunatakiwa kuifanya ya kupambana kupata pointi tatu,"amesema Mwanahamisi.

Awali, Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya amesema maandalizi ya mchezo wa marudiano wa Serengeti Lite Women’s Premier League (SLWPL) dhidi ya Yanga Princess utakaopigiwa leo Uwanja wa Uhuru yamefanyika vizuri.

Makanya amesema, kikosi kiliingia kambini moja kwa moja baada ya mchezo dhidi ya The Tigers Queens ambao waliibuka na ushindi wa mabao 7-0.

“Mchezo utakuwa mgumu Derby siku zote haina mwenyewe na tofauti yetu ya pointi moja dhidi ya Fountain ndio inatufanya tuzidi kuwa makini na mchezo huu, lengo letu ni kuhakikisha tunachukua ubingwa kwa mara ya nne mfululizo,”amesema Makanya.

Makanya amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu ili kutimiza malengo ya kuchukua ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.

“Ni mechi kubwa na muhimu kwetu, tunahitaji sana kupata ushindi na hilo litakuwa gumu kama tusipopata sapoti ya mashabiki wetu, ndio maana tunawasisitiza waje kwa wingi,”amesema Makanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news