NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi ameridhishwa maendeleo ya miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Ofisi hiyo ambapo amesema kukamilika kwake kutawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (wa kwanza) akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali linalojengwa Kisasa, Jijiji Dodoma alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maeneo ya miradi ya ujenzi iliyopo chini ya Ofisi hiyo.(Picha na OWM).
Dkt. Yonazi ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa maeneo yenye miradi ya ujenzi iliyopo chini ya Ofisi hiyo na kuwataka wakandarasi kuongeza juhudi ili majengo hayo yakamilike kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
Amesema uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa .Dkt. Samia Suluhu Hassan kutekeleza miradi hiyo mikubwa ni kuhakikisha shughuli za Serikali zinafanyika katika mazingira yenye ubora na kuhudumia wananchi kwa weledi.
“Tumefanya ukaguzi wa majengo ya Kituo cha Operesheni ya Maafa, jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, jengo la Idara ya Kupiga Chapa Kisasa na jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mtumba na maendeleo ni mazuri,”amesema Dkt. Yonazi.
Pia amewahimiza wakandarasi kuhakikisha wapata vifaa kwa wakati ili ujenzi huo kufanyika ndani ya muda uliopangwa pamoja na wasimamizi kusimamia kikamilifu kuhakikisha majengo hayo yanakuwa na ubora unaotakiwa.
“Tumetoa angalizo kwamba lazima usimamizi uwe mzuri na majengo yakamilike kwa wakati, zipo changamoto mbalimbali kama vifaa lakini tumekubaliana wakandarasi wafuatilie vifaa ili majengo haya yatumike na watumishi wa Serikali na wakae sehemu mmoja kutumikia wananchi kwa pamoja,”ameeleza Katibu Mkuu huyo.
Aidha amewahimiza kuongeza ubunifu wa utendaji kazi hatua itakayosaidia kuhamasisha kazi kufanyika kwa mwamko na ubora zaidi.
Kwa upande wake Mkadiriaji Majenzi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi Mhandisi Saudeni Anania ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana nao huku akisema wanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya umaliaziaji ujenzi.