NA DIRAMAKINI
KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji ameitaka Kamati ya Udhibiti na Usimamizi Ujenzi (DCU) kutochelewesha kutoa vibali vya miradi ili ujenzi wa miradi hiyo utekelezwe kwa muda uliyotakiwa.
Dkt. Mngereza aliyasema hayo jana baada ya kupokea maoni ya wajumbe katika kikao cha 74 cha kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alisema maombi ya vibali vya miradi yasikae muda mrefu yawe yamejibiwa ili ujenzi wa miradi uanzwe kutekelezwa kwa wakati.
Pia aliitaka kamati hiyo kuanzisha utowaji wa vibali vya ujenzi kwa njia ya mfumo wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) ambapo utawezesha kamati hiyo kufanya majukumu yao ipasavyo.
“Vibali vya miradi visikae muda mrefu havijatolewa, kuwe na time frame, pia kuwe na land forum, mfikirie kuanzisha mfumo wa ICT na mkimfanye kazi kwa mashirikiano itasaidia kupunguza malalamiko,”amesema Dkt.Mngereza.
Aidha Dkt. Mngereza alisisitiza umuhimu wa kuitumia ardhi vizuri. Alisema ardhi ikitumika kwa mujibu wa matumizi yake ndio maendeleo ya kiuchumi Zanzibar yatafikiwa kwani mipango bora katika sekta ya ardhi ni kwaajili ya huduma za makaazi na kiuchumi ndio adhma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Sambamba na hayo Katibu Mkuu huyo alisema wizara yake itajenga nyumba za Maendeleo sehemu mbali mbali ambayo wameyaainisha ila hakusema eneo lipi litakuwa la kwanza kujengwa, bali alieleza muda sio mrefu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi itasaini mkataba wa ujezi wa nyumba za mkopo wa bei nafuu.
Naye Mkurugenzi Idara ya Ardhi kutoka Kamisheni ya Ardhi Zanzibar Ndg. Mtambua Hamziji Haji aliunga mkono hatua ya kuanzishwa Jukwaa la Ardhi (Land Forum) kwani litaweza kusaidia watendaji wa sekta ya hiyo kuzungumza kwa kina na kila mmoja atazungumza kinachomhusu katika majukumu yake.
“Bora kuwe na Land forum kwasababu DCU wao wanalenga kukusanya mapato na kusahau matumizi bora ya ardhi wakati ardhi ikitumika vizuri mapato yatapatikana kwa mujibu wa matumizi yake, sisi Kamisheni ya Ardhi tunasimamia matumizi bora ya ardhi,”amesema Haji.
Kwa upande wao wajumbe wa Kamati ya Udhibiti na Usimamizi Ujenzi (DCU) wamelalamikia ukosefu wa fedha katika kutekeleza majukumu yao kwani wanakusanya fedha kutokana na utowaji wa vibali vya ujenzi na kuingiza katika mfuko mkuu wa Serikali lakini fedha hazirudi (return) hali ambayo inapelekea kutokutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kikao hicho cha Kamati ya Udhibiti na Usimamizi Ujenzi (DCU) kimeandaliwa na Mkurugenzi Mipango Miji Muchi Juma Ameir ambae ndie mwenyekiti wa kamati hiyo.