Elimu ya mtoto wa kike nchini kuimarishwa

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) imelenga kuinua ubora wa elimu kwa kuongeza ushiriki na ufaulu wa watoto wa kike katika masomo ya sanyansi na hisabati.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mheshimiwa Angellah Kairuki ameyasema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na kaimu afisa elimu mkoa wa Kigoma,Bw. Shukuru Kalegamye wakati wa kufunga kongamano la wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari kwa mikoa ya Kigoma, Songwe na Tabora lililofanyika mjini Kasulu mkoani Kigoma.

Mhe.Kairuki amesisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania imeweka msukumo maalumu kwa wasichana kusoma masomo ya sayansi na hisabati na kwamba uanzishwaji wa midahalo kwa wanafunzi na walimu wa Sanyansi ni sehemu ya mipango ya kutambua changamoto, vikwazo na kufahamika kwa fursa zilizopo katika masomo hayo kwa watoto wa kike.

Amebainisha kuwa, serikali tayari imeanza kuzitambua changamoto ambazo ni vikwazo ikiwemo baadhi ya wazazi kuwashawishi watoto kutosoma masomo hayo, walimu kukosa mbinu rafiki na shirikishi pamoja na kasumba ya jamii kuona kuwa masomo ya sayansi ni magumu na kwamba wasichana hawayawezi ukilinganisha na wavulana.

“Natoa wito kwa jamii, wazazi na wanafunzi wenyewe wahamasike na wapende kusoma masomo ya sayansi na sisi tuitaendelea kuwawezesha walimu kwa kuwajengea uwezo ili wawe na maarifa ya kutosha ya kufundisha masomo ya sanyansi,” amesema Mheshimiwa Kairuki kupitia hotuba hiyo.

Mheshimiwa Kairuki ameagiza watendaji wote wa serikali, maafisa elimu na wadau wengine kushirikiana kutekeleza mikakati yote ya kuwezesha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi na hisabati sambamba na kusimamia mpango wa kila mtoto wa kike anayebalehe asome na kufanikiwa.

Kwa upande wake mtaalam wa elimu kutoka UNICEF, Bw. Ayoub Kafyulilo amepongeza serikali kwa kushirikisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza mpango huo ambao utazalisha wanasayansi, tekonolojia na uhandisi kwa watoto wa kike.

Amesisitiza kuwa, maoni na ushauri wote uliotolewa na wakufunzi pamoja na watoto wenyewe ni msingi mzuri kwa shirika hilo pamoja na wadau wengine ili kukamilisha utafiti wa nini ni kikwazo cha watoto wa kike kutosoma masomo ya sayansi na hisabati yanatafutiwa ufumbuzi.

Kwa upande wao watoto hao kutoka mikoa ya Songwe, Kigoma na Tabora waliweka bayana katika mdahalo wao kuwa, wasichana wengi hawasomi masomo ya sayansi kutokana na kukatishwa tamaa na jamii pamoja na walimu.

Walibainisha kuwa, baadhi ya wazazi hawaoni umuhimu na wala hawawahimizi watoto wao wa kike kutokana na dhana tu kwamba masomo hayo nimagumu na kwamba wavulana pekee ndio wenyeuwezo wa kusoma, huku wengine wakitaja kuwa uchache wa walimu wa sayansi na ushawishi hasi wa shuleni nimoja ya vizuizi.

Awali mwakilishi wa OR-TAMISEMI,Dkt. Yangson Mgogo alibainisha kuwa mdahalo huo wa wanafunzi kuhusu masomo ya sanyansi na hisabati kwa mikoa ya Songwe, Kigoma na Tabora ni hatua za awali za utekelezaji wa mpango wa kuhakikisha Watoto wa kike wanasoma masomo hayo kufuatia kuwepo kwa matokeo ya awali ya tafiti zilizoonesha kuwa wasichana wako nyuma ukilinganisha na wavulana.

Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Elimu nchini, kiwango cha ufaulu kwa wasichana katika mikoa hiyo kilikuwa chini katika masomo hayo kwa wastani wa asilimia kati ya 15 hadi 88 nyuma ya wavulana kwa Mkoa wa Kigoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news