Fahamu chimbuko la Siku ya Wanawake Duniani

NA MWANDISHI MAALUM

MACHI 8, kila mwaka ni Siku ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi tarehe 8 Machi 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuridhia siku hiyo kutumika kama siku rasmi ya kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake ikiwemo kuongeza chachu katika harakati za mapambano ya usawa wa kijinsia kwa wanawake na wanaume katika jamii. 
Maadhimisho hayo kila mwaka hubeba ujumbe mahususi kama ilivyo kwa mwaka huu yamebeba ujumbe usemao, “Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia” 

Chimbuko la siku ya Wanawake Duniani, ilianza kupata umaarufu ukanda wa magharibi baada ya mwaka 1977 kufuatia azimio la baraza la umoja wa mataifa kuridhia Machi 8 kuwa ni siku ya umoja wa mataifa ya haki za wanawake na amani duniani, zaidi ya nchi 100 zinaadhimisha siku ya wanawake duniani na baadhi ya nchi wameitangaza kama siku rasmi ya mapumziko. 

Lengo kuu la siku hii ni kuonesha mapenzi na shukrani kwa wanawake na kutambua changamoto wanazopitia katika maeneo mbalimbali duniani na kuzitafutia ufumbuzi kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa amani na utulivu. 

Mwaka 1908 kulitokea mtafaruku na mjadala mkubwa kuhusiana na wanawake, ikumbukwe miaka hiyo kulikuwa na unyanyasaji na kutokutambulika kwa haki za wanawake hali iliyopekea wanawake kuanza kupaza sauti na kuendesha kampeni ili kuleta mabadiliko. 

Kutokana na hali hiyo, mwaka huo 1908 wanawake 15,000 waliandamana jijini New York wakitaka kupunguzwa kwa masaa ya kazi, malipo mazuri na haki ya kupiga kura. 

Mwaka 1909 ikiambatana na azimio la Chama cha Kijamaa cha America (Socialist Party of America) walipitisha Siku ya Kitaifa ya Wanawake (National Women’s Day) nchini Marekani tarehe 28 February. Wanawake waliendelea kusherehekea siku hii mpaka siku ya mwisho ya Jumapili ya Februari mwaka 1913. 

Mwaka 1910 mkutano wa pili wa kimataifa kwa wanawake wafanyakazi (International Conference of Working Women) ulifanyika mjini Copenhagen, Denmark. 

Katika mkutano huo, mwanamke aitwaye Clara Zetkin ambaye alikuwa kiongozi wa Women Office kwa chama cha Social Democratic nchini Ujerumani aliwasilisha wazo la Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Pendekezo lake kuu ilikuwa ni kila nchi duniani kila mwaka washerehekee siku moja ili kutambua mahitaji ya wanawake. 

Wanawake takribani 100 kutoka mataifa 17 walihudhuria mkutano waliwasilisha vyama vya wafanyakazi vya ushirika na kijamaa. 

Bunge la Finland ambalo wakati huo lilikuwa na wanawake watatu, walipitisha wazo la Clara ambalo lilichangia kuanzishwa kwa siku ya wanawake duniani. 

Tarehe ambayo mgomo wa wanawake ulianza kwa kalenda ya Juliana, ambayo wakati huo ilikuwa ikitumika nchini Urusi, ilikuwa Jumapili Februari, 23. Siku hii katika kalenda ya Gregorian ilikuwa Machi 8. Huu ndio wakati ambapo sasa inaadhimishwa kama siku ya mapumziko nchini Urusi na nchi zingine takribani dazeni mbili 

Tarehe 8 Machi 1995, uliitishwa Mkutano wa nne wa wanawake duniani (4th World Conference on Women) ukiwa na kaulimbiu ya vitendo kwa usawa, maendeleo na amani. 

Mkutano ulifanyika katika mji wa Beijing, China na ndiyo chanzo cha kuitwa Beijing Conference. Mama Gertrude Mongella kutoka Tanzania alipata heshima ya kuongoza kikao hiki kama Katibu mkuu wa mkutano. 

Mkutano uliambatana na hotuba kutoka kwa wanawake wenye ushawishi kama Hilary Clinton na Mother Teresa ambaye sehemu ya hotuba yake alinukuliwa akipinga suala la utoaji mimba ambapo baadhi ya mataifa walianza kuruhusu sheria ya utoaji mimba. 

Mkutano wa Beijing unatazamwa kama moja ya mikutano mikubwa iliyoweza kuamsha hali ya wanawake kudai haki zao za msingi. Hotuba ya Bi Hilary Clinton kwa kiasi kikubwa iliweza kushawishi wanawake kuendesha harakati za kupigania haki zao. 

Maazimio ya mkutano huo yalipelekea kubadilika kwa hali ya wanawake katika nyanja tofauti ikiwemo umaskini, elimu, afya, ukatili, siasa na maamuzi. Mama Gertrude Mongella baada ya mkutano wa Beijing ameendelea kuwa alama kubwa ya kupigania haki za wanawake na amekuwa ni mfano wa kuigwa kwa wanawake na mabinti wengi ndani na nje ya Tanzania. 

Kila mwaka Machi 08, Umoja wa Mataifa husheherekea haki zilizopatikana kwa bidii za wanawake na kuangazia changamoto ambazo bado ziko mbele katika kukomesha ubaguzi wa kijinsia katika karibu nyanja zote za maisha. 

Dkt.Maxime Houinato, mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake katika kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, alipokuwa anahojiwa na BBCalisema kuwa Wanawake na wasichana wanapitia athari kubwa zaidi za mabadiliko ya tabia nchi, utafiti wa Umoja wa Mataifa unaonesha kuwa wanawake na wasichana hufa kwa idadi kubwa katika majanga ya asili.

”Kwa mfano, asilimia 95 ya waliofariki katika mafuriko ya visiwa vya Solomon 2014 walikuwa wanawake, 55% ya waliofariki katika tetemeko la ardhi la 2015 nchini Nepal walikuwa wanawake na 59% ya waliokimbia makazi yao kufuatia Kimbunga Idai mwaka 2019 nchini Malawi walikuwa wanawake,” UN Women imesema kwenye tovuti yake. 

Kwa upande wa nchi za Afrika, siku ya wanawake duniani inaadhimishwa kama sikukuu ya umma katika nchi saba za Afrika. Hii ni pamoja na Eritrea, katika kutambua mchango mkubwa ambao wanawake na wasichana walitoa – kama wapiganaji – katika mapambano ya muongo mzima wa uhuru wa nchi hiyo. 

Mataifa mengine ya Afrika ambayo yametangaza tarehe 8 Machi kuwa siku ya mapumziko ni Angola, Burkina Faso, Guinea-Bissau, Sierra Leone ,Uganda na Zambia.Huko Madagascar, ni siku ya mapumziko kwa wanawake pekee. 

Baadhi ya nchi za Kiafrika zina Siku yao ya Wanawake – Afrika Kusini inaadhimisha kama siku ya mapumziko tarehe 9 Agosti kwa heshima ya wanawake 20,000 walioandamana siku hiyo mwaka 1956 kupinga sera za kibaguzi ya utawala wa wazungu wachache uliokuwa madarakani kwa wakati huo. 

Ingawa bado kuna mengi yanahitajika kufanywa ili kufikia usawa wa kijinsia.Wanawake barani Afrika wamepata mafanikio makubwa ambapo takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2021 zinaonesha kuwa Rwanda ina idadi kubwa ya wanawake bungeni – 61%, ikifuatiwa na Cuba na Bolivia zenye 53% kila moja na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa 50%.Afrika Mashariki na Kusini ndizo zenye uwakilishi mkubwa zaidi wa wanawake bungeni katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara – 32% kufikia Disemba 2020, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa 24.5%. 

Nchi ya Tanzania pia ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki katika siku ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa kuhakikisha kila mwanamke anashiriki kwa namna moja au nyingine kuadhimisha siku adhimu kama hii. 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dr. Dorothy Gwajima amesema kwa mwaka huu katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani wamelenga katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na ubunifu wazalishaji wa ndani hususani wanawake. 

Dr.Gwajima alisema kwa kuwa wanawake wajasiriamali ni kundi muhimu katika kukuza uchumi wa pato la taifa, ameelekeza mikoa na wadau wote kwamba katika kuwaunga mkono, vazi la batiki litumike kama sare rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu. 

Siku ya wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka kuanzia Machi 1 na kufikia kilele Machi 8 ambapo kwa mwaka huu yanafanyika kila mkoa yakiratibiwa kupitia ofisi za wakuu wa mikoa na halmashauri zote nchini. 

Jeshi la Polisi Tanzania ni miongoni mwa idara zilizopo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo nayo kila mwaka inashiriki katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa kujikita katika kutekeleza majukumu mbalimbali na kutoa huduma mbalimbali katika Jamii. 

Kwa kuonesha umakini na kuchukulia kwa uzito siku hii ya wanawake dunia Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-Net) uliopo chini ya Mwenyekiti wa mtandao huo, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda ambaye pia ni Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu ukiwa na lengo la kujengeana uwezo na kujiamini kutekeleza majukumu yao katika masuala ya kimaendeleo na mambo yanayo mhusu mwanamke, Kumfanya mwanamke kutambua haki na wajibu wake, kuelimishana juu ya masuala ya kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia pamoja na kupata uelewa juu ya masuala ya rushwa na namna ya kuepukana nayo. 

Kila mwaka Polisi wanawake Tanzania kila mkoa kupitia mtandao huo, wamekuwa wakiadhimisha siku hii adhimu kwa kutoa elimu kwenye vyombo vya habari inayohusu masuala ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto, Kutembelea shule mbalimbali za wasichana na kuwapa elimu ya maadili mema, matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii na namna ya kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ya vitendo vya ukatili wanavyotendewa pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa ya vitendo vya ubakaji na ulawiti ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mhusika. 

Aidha, Mtandao wa Polisi wanawake katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani wamekuwa wakitoa misaada katika vituo mbalimbali vya watoto yatima na waishio katika mazingira magumu, Kushirikiana na wananchi katika kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali, Kutembelea wagonjwa katika hospitali na kutoa misaada na elimu ya masuala ya uhalifu pamoja na kutoa elimu ya namna ya kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu katika maeneo ya sokoni, mashuleni, maeneo ya kuabudia, stendi za mabasi na daladala pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi. 

Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani kwa mwaka 2023 Jeshi la Polisi Tanzania limeadhimisha kwa Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma kushirikiana na Askari wa kike kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani Dodoma kufanya matembezi ya mshikamano katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. 

Matembezi hayo yaliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule na kuhusisha vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoa wa Dodoma ambapo yalianzia katika Viwanja vya Nyerere Square mpaka Chinangali Park ambapo yaliambatana na utoaji wa mada mbalimbali. 

Katika Maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka kujenga utaratibu wa kukutana mara kwa mara ikiwezekana kila baada ya miezi mitatu ili kuimarisha umoja baina yao. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TPF Net Kamishna wa Polisi Suzan Kaganda ambaye pia ni Kamishna wa Kamisheni ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu ndani ya Jeshi la Polisi alisema ushirikiano katika vyombo vya usalama ni muhimu na kupitia matembezi hayo na mada zitakazotolewa zitawaongezea maarifa Askari hao wa kike. 

Pia, katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani tarehe 08.03.2023 Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-Net) Machi 03, 2023 wametembekea kituo cha kulelea watoto yatima na watu wenye uhitaji maalumu huko Hombolo Wilaya ya Dodoma Jijini Dodoma. 

Wakiwa katika kituo hicho wametoa misaada kwa watu wenye mahitaji maalum wanaolelewa hapo ambao ni Wazee na Watoto yatima.Kituo hicho kinasimamiwa na Masista wa shirika la Mama Teresa 
Akizungumza kwa niaba ya Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-NET) Makamu Mwenyekiti Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Maria Nzuki amesema wameona ni vyema kutoa msaada huo kwani ni utamaduni kwa Jeshi la Polisi kutoa misaada kwa vituo vya kulelea watoto yatima na makundi yenye uhitaji na kutoa mwaliko kwa wananchi kuwa na desturi ya kutembelea na kutoa misaada katika vituo hivyo. 

Mkuu wa kituo hicho cha Mama Teresa, Sista Prudencia ambaye ni Sista mkuu amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwatembelea na kwa msaada wao na kusema kuwa imekuwa faraja na furaha kwao. 

Kupitia msaada huo amesema itawasaidia katika kuwatimizia mahitaji wahitaji maalumu hasa kwa watoto yatima na kulikaribisha tena Jeshi la Polisi kuwatembelea mara kwa mara. 

Machi 8, 2023, Maofisa, Wakaguzi na askari wanawake wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF – NET) Kamishna wa Polisi Suzan Kaganda wameshiriki katika maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani ambayo kwa Mkoa wa Dodoma yamefanyika katika wilaya ya Kondoa yenye kaulimbiu isemayo, “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia katika kuleta Usawa wa Kijinsia”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news