NA DIRAMAKINI
KAMPUNI ya Grumeti Fund kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imewakumbusha vijana wa kiume wilayani Serengeti mkoani Mara kutekeleza majukumu yao katika jamii zinazowazunguka.
Akizungumza katika Kongamano la Vijana wa Kiume lilofanyika Machi 25, 2023 na vijana waliotoka shule za Sekondari Serengeti na Nyichoka, mgeni rasmi Mwalimu Wandere Pamba Rwakatare ambaye ni Afisa Elimu Sekondari wa Bunda Vijijini, amewakumbusha vijana hao kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo katika jamii ikiwemo kuwalinda na kuwapa vipaumbele vijana wa kike sambamba na kujisimamia ili waweze kutimiza ndoto zao.
"Vijana wa kiume tunawajibu wa kutimiza ndoto zetu,lakini pia tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba binti unayeishi naye katika jamii yako naye anatimiza ndoto zake, elimu unayoipata ikusaidie kuionesha jamii ambayo unaishi nayo kwamba tunazo mila ambazo zinamkandamiza mtoto wa kike ambazo kwa sasa hazistahili,’’ amesema Mwalimu Rwakatare.
Mwalimu Wandere Pamba Rwakatare ameongeza kuwa, "mabinti katika ngazi za elimu ya chini hawafanyi vizuri kutokana na mikandamizo ambayo tunayo katika jamii, lakini mtu ambaye anastahili kumlinda huyo binti ni wewe kaka yake, wewe ni jeshi linalomzunguka binti,uwe askari wake akiwa shuleni ,nyumbani au njiani ili tunapotaka kufikia ndoto zetu tufikie kwa pamoja,’’amesema Mwalimu Rwakatare.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamiii ya Kampuni ya Grumeti Fund, Frida Mollel amewasihi Vijana hao kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika kutimiza majukumu yao
‘’Wanaume wana nguvu kubwa sana katika ajenda ya kumuwezesha binti kufikia ndoto zake kuanzia mdogo, wakiwa mashuleni, makazini lakini pamoja na majumbani.Tupige vita mila na desturi zisizo na tija,’’amesema Frida.
Frida ameongeza kuwa, badala ya mtoto wa kiume na wa kike kuwa washindani ni vema kuinuana ili kwenda sambamba, amehimiza pia vijana kutojiingiza katika matendo maovu yanayosababishwa na makundi rika na kuiga tabia zinazoletwa na utandawazi. Huku akiwahimiza kwenda kutekeleza yote waliyojifunza katika kongamano hilo.
Nao vijana walioshiriki katika kongamano hilo wameishukuru Kampuni ya Grumeti Fund kwa kutoa elimu na kuahidi kuwa mabalozi wazuri na kutekeleza yote waliyoelekezwa katika kongamano hilo kwa faida yao na jamii.