NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amewaomba wakazi wa Jiji la Dodoma kuzingatia usafi wa mazingira kila siku ili kuliweka Jiji katika Hali ya usafi ili kuendelea kuipa hadhi na mvuto wa makao Makuu na kuepuka magonjwa ya mlipuko.



Aidha, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Bw. Dickson Kimaro amesema hadi sasa wamekusanya zaidi ya shillingi milioni moja kwa wale wote wasioshiriki katika zoezi Hilo.
"Kwa wananchi ambao hawatekelezi Sheria ya kufanya usafi huwa tunawatoza faini na hadi kufikia hii leo zaidi ya Milioni Moja zimekusanywa Kama faini kwa wale wote wanakutwa wakiendelea na shughuli binafsi muda ambao umetengwa kwa ajili ya usafi,"amesema Kimaro
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwaja ambapo ndipo zilipo ofisi za kata, Bw. Athumani Makuka amekiri kuwachukulia hatua wale wote wasiozingatia kanuni na taratibu zilizowekwa katika kutimiza adhma ya kuliweka Jiji katika Hali ya usafi muda wote.
"Ushiriki wa wananchi ni mzuri na unatia moyo tangu tulipoanza masuala ya usafi na tumekuwa tukiwaomba Taasisi mbalimbali za mazingira kushirikiana na sisi na wamekuwa wakituunga mkono katika kulitekeleza hili.
"Tunawachukulia Sheria wale wote wasio hudhuria siku ya usafi ambayo ni jumamosi ikiwa ni kutozwa faini na kufikishwa kwenye Ofisi ya Mtendaji wa kata na tunashirikiana na polisi jamii katika kulitekeleza agizo hili la usafi wa mazingira na kuliweka Jiji letu katika Hali ya usafi,"amesema Makeka