HII MIKOPO UMIZA:Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Hassan Ngoma alitoa wito kwa walimu kupunguza idadi ya mikopo wanayokopa katika taasisi za fedha hasa zile zenye riba umiza ili kujinusuru na umaskini.

DC alitoa wito huo baada ya walimu kuibua malalamiko kwamba wanaishi maisha magumu kwa sababu wanalipwa mshahara mdogo huku lawama zikielekezwa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kudaiwa kuchangia ugumu huo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi Mkutano Mkuu wa Nusu Muhula wa Chama cha Walimu Wilaya ya Ruangwa (CWT), DC Ngoma alielezwa kusikitishwa na mienendo ya baadhi ya walimu wanaosalimisha hadi kadi zao za benki kwenye taasisi za fedha ili kukopa fedha zinazowalipisha riba za asilimia 60 hadi 70 kwa mwezi.

“Unakuta mwalimu mmoja ana deni benki, Vicoba na michezo zaidi ya miwili ambayo inamlazimu kulipa hadi shilingi elfu kumi kwa siku, achilia mbali yale madeni ya anayolipa kila mwisho wa mwezi. Katika hali hiyo ni mwalimu gani atapata utulivu wa nafsi?,” mteule huyo wa Rais alihoji.

Alisema, inafikirisha mno kuona mwalimu ana madeni mengi na makubwa kiasi hicho, lakini bado serikali na jamii inamtegemea afundishe vizuri na kwa weledi ili kumpa matokeo chanya wanafunzi.

DC Ngoma aliwataka walimu kukubali kubadili mifumo ya maisha yao kwa kuanza kulipa madeni yao yote na kuanza upya ili kupitia mishahara wanayolipwa waweze kuwekeza katika biashara na hatimaye kuinua hali za maisha yao.

Alisema Serikali inawategemea katika kuelimisha taifa na kwamba wakiendelea kukopa mikopo isiyo na tija, hawataweza kufundisha kwa weledi kwa sababu ya kuhelemewa na madeni.

Wakati huo huo, hivi karibuni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kwa sasa hakuna sera waliyopitisha ambayo inataka watoa huduma ndogo za fedha kutoza riba zaidi ya asilimia 3.5 kwa mwezi au 42 kwa mwaka huku ikiwataka wananchi kutokopa fedha kwa mtoa huduma ambaye hana leseni kutoka BoT, kwani huyo ni miongoni mwa wahalifu.

Kaimu Msimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka Benki Kuu,Mary Ngasa aliyasema hayo Februari 27, 2023 katika semina kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini kuhusu majukumu ya msingi ya BoT na namna Benki Kuu inasimamia watoa huduma ndogo za fedha.

Semina hiyo iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu jijini Dar es salaam, ilifunguliwa na Naibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael kwa niaba ya Gavana, Emmanuel Tutuba.

Wakati wa majadiliano baada ya kuwasilisha mada kuhusu Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Ngasa alifafanua kuwa,Benki Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutoa sheria,kusajili,pia kutoa kanuni na miongozo kuhusiana na sekta hiyo.

"Kama nilivyosema, wanapokuja (watoa huduma) huku kusajili, tunapitia huduma zao zote. Tunapitia mpaka riba, na kwa sasa hakuna sera tuliyopitisha yenye riba zaidi ya asilimia 3.5 kwa mwezi,hivyo ambaye anatoa riba zaidi ya hiyo, tufahamisheni.

"Ina maana kwa mwaka ni asilimia 42 na kwa mwezi ni asilimia 3.5. Anayetoa kinyume na hapo na ana leseni ya Benki Kuu anakwenda kinyume cha leseni ya Gavana, yaani hilo ni kosa kubwa mno na uwezekanao wa kunyang'anywa leseni upo,"alifafanua Bi.Ngasa.Pia alisema, anayetoa mikopo bila kuwa na leseni ya Benki Kuu anakwenda kinyume cha sheria na ni mhalifu.

"Anayetoa mikopo bila leseni anakwenda kinyume cha sheria za nchi, ndiyo maana tunasema, hili suala la fedha elimu itolewe kwa watu wengi. Usiende kukopa hela kwa mtu ambaye hana leseni ya Benki Kuu,unapoenda kukopa cha kwanza hakikisha ana leseni ya Benki Kuu ambaye hana leseni ni mhalifu na anavunja sheria,"amefafanua Ngasa.

Alisema, katika tovuti ya Benki Kuu wanachapisha orodha ya watoa huduma ndogo za fedha wote ambao wamepewa leseni.

"Suala la msingi na suala muhimu, mtumiaji wa huduma ndogo za kifedha,jamani tusiweke shida mbele, shida zipo...tuwe na mazoea ya kuwafahamu watoa huduma ndogo za fedha kabla ya kufikwa na matatizo, kuna haki za msingi ambazo mwananchi anapaswa kuzifahamu ili kuepuka udanganyifu.

"Na utafute mkataba na uusome na uelewe kabla ya kufanya maamuzi, ingia ukiwa unafahamu vigezo na masharti kabla ya kufanya maamuzi, kwa hiyo mwenye riba zaidi ya hiyo tuleteeni ili tushughulike naye,"amefafanua Ngasa.

Ngasa amesema, hadi sasa kuna jumla ya taasisi za watoa huduma ndogo za fedha zinazofikia 1,000 ambazo zimesajiliwa na BoT kwa Tanzania Bara.

Akizungumzia kuhusu Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Na.10 ya mwezi Novemba 2018 amesema, Serikali iliitunga ili kusimamia biashara ya huduma ndogo za fedha na kuhamasisha ukuaji na uendelezaji wa sekta hiyo.

“Ibara ya 12 ya sheria hiyo imeipa mamlaka Benki Kuu ya Tanzania kusajili, kusimamia na kudhibiti biashara ya huduma ndogo za fedha Tanzania Bara, lengo kuu hasa ni kuwasaidia wananchi kuepuka changamoto za udanganyifu zilizokuwa zikiwakumba kabla ya kuanzishwa kwa sheria.

"Pia Ibara ya 16 ya sheria hiyo imetoa katazo kwa mtu au taasisi yeyote kufanya biashara ya kutoa huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania inayoruhusu kufanya biashara hiyo,”amesema.

Amesema, sheria imetoa tafsiri juu ya huduma ndogo za fedha kuwa ni biashara inayojumuisha kupokea fedha, kama amana au riba kutokana na amana au mkopo na kuikopesha kwa wanachama au wateja, kupokea amana na kutoa mikopo au huduma ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo, kaya au mtu mmoja mmoja.

Ngasa aliwataka watoa huduma kufuata maelekezo ya Benki Kuu na kanuni zilizowekwa katika uendeshaji wa shughuli zao ikiwa ni pamoja na kutoa hati ya mkataba kwa maandishi kwa watumiaji wa huduma husika.

Mbali na hayo aliwataka watumiaji wa huduma wanapopewa huduma huku wakiweka dhamana mbalimbali kuhakikisha kuwa, wanarejesha kwa wakati mikopo kama walivyokubaliana na watoa huduma ili kuepuka changamoto mbalimbali ambazo wanaweza kukumbana nazo. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo. Endelea;


1.Hii mikopo umiza, iache kuwaumiza,
Wito msijepuuza, yale wanawaeleza,
Unapokopa chunguza, kuyajua ya kukwaza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

2.Jambo la kujizoeza, mkopo hujauwaza,
Mwenyewe kijiongoza, yale wataka timiza,
Hesabu za kuongeza, utakavyourejeza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

3.Usije kujilegeza, masharti kuchunguza,
Huko ndiko wanaweza, wewe wakakubamiza,
Huko wakikumaliza, utabaki wajiliza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

4.Kurudisha unaweza, mkopo unauwaza?
Masharti wayaweza, au unajimaliza?
Hayo ni mambo chunguza, usije ukajiliza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

5.Ukikopa nakujuza, namna kulipa waza,
Siyo pesa wamaliza, halafu unateleza,
Mkopaji wamkwaza, jua atakukimbiza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

6.Kingine cha kuchunguza, hata pia kuuliza,
Mkopeshaji kuweza, ya kwamba anajiweza,
Ana leseni uliza, au anabangaiza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

7.Kama anabangaiza, kwake acha jisogeza,
Hapo tena ukiweza, mamlaka kueleza,
Kwani wameshakataza, wasijikujiingiza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

8.Vinginevyo kujiliza, mwenyewe waendeleza,
Kwa sababu wapuuza, haya tunakueleza,
Hivyo wajiangamiza, shida zako waongeza,
Kama hutakurupuka, mikopo siyo kikwazo.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news