HUDUMA NDOGO ZA FEDHA ZINGATIENI SHERIA

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Na.10 ya mwaka 2018 mwezi Novemba 2018 ili kusimamia biashara ya huduma ndogo za fedha na kuhamasisha ukuaji na uendelezaji wa sekta hiyo.

Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha zilitangazwa na Waziri mwenye dhamana ya Fedha kuanza kazi rasmi mnamo Novemba Mosi, 2019. Pia, kanuni zilitangazwa kwenye gazeti la Serikali mnamo tarehe 13 Septemba 2019 GN. Na.675.

Aidha, kufuata Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 kuna manufaa makubwa kwa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kutokana na sababu za msingi.

Miongoni mwa sababu hizo ni kikundi kutambuliwa kisheria kama taasisi huru inayoweza kumiliki au kuuza mali, kuwa na ulinzi kisheria linapotokea tatizo, kuboresha uhusiano na watoa huduma rasmi za fedha ili wanakikundi waweze kunufaika na huduma mbalimbali za fedha za gharama nafuu.

Nyingine ni kuongeza usalama wa fedha zinazochangwa na wanachama endapo vikundi vitahifadhi michango ya wanachama kwenye akaunti benki na vikundi vilivyosajiliwa vitafaidika na miradi mbalimbali ya Serikali inayolenga kuimarisha vikundi nchini.

Pia, faida muhimu za sheria hii kwa vikundi vya kijamii ni kwamba taarifa za wanachama wao na historia ya mikopo itapatikana kwenye mifumo ya ubadilishanaji taarifa za wakopaji.

Hii inasaidia katika kuwajulisha wana kikundi juu ya wanachama uaminifu, wanaofaa kujiunga na vikundi na kupewa huduma.

Vile vile, sheria na kanuni za Huduma Ndogo za Fedha zinaeleza kuwa kikundi cha kijamii cha huduma ndogo za fedha kinaweza kuundwa na watu 10 hadi 50, ambao wana lengo la pamoja.

Wanachama wanapaswa kukutana ili kukubaliana juu ya uundaji wa kikundi, kujiwekea malengo,kuunda katiba, na kamati ambayo itawezesha uanzishwaji wa kikundi.

Kanuni hizo pia zinavitaka Vikundi vya Kijamii Vya Huduma Ndogo kuwasilisha maombi ya usajili kwa mamlaka husika ya Serikali za mitaa kwa fomu maalumu ambayo itatolewa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ambayo imekasimishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kusimamia vikundi nchini.

Maombi yataambatana na nyaraka kadhaa ikiwemo nakala mbili za katiba zilizosainiwa na wanachama wote, nakala moja ya taarifa za mkutano wa kwanza wa uundaji wa kikundi uilosainiwa na washiriki wote wa mkutano wa awali.

Maazimio ya wanachama kuunda na kusajili kikundi cha kijamii, muundo wa kikundi uliopendekezwa na majina ya viongozi waliopendekezwa na kuidhinishwa na wanachama katika mkutano wa uundaji wa kikundi.

Nyingine ni orodha ya wanachama, ikiwa idadi ya wanachama ni 10 hadi 50 kulingana na kanuni, ushahidi wa michango ya wanachama wa kikundi cha awali iliyowekwa katika akaunti ya kikundi, barua ya utambulisho kutoka ofisi ya serikali ya kijiji, mtaa au kata kuanzisha kikundi na nyaraka au taarifa nyingine zozote zinazofaa.

Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha inalenga kuimarisha vikundi vya kijamii, kwani kabla ya utekelezaji wa sheria hii, sekta ndogo ya fedha ilikuwa inafanya kazi bila kudhibitiwa au kusimamiwa, na kuacha mianya uhalifu mwingi, upotevu, na udanganyifu mkubwa baina ya washiriki wa sekta hii ya huduma ndogo za fedha.

Kupitia sheria hii, watumiaji wa huduma ndogo za fedha wanalindwa na sheria dhidi ya wahalifu wowote, na kuleta muundo na mpaangilio bora ndani ya sekta ndogo ya Huduma Ndogo za Fedha nchini.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ukifuata sheria na kanuni katika utoaji huduma ndogo za fedha si tu kwamba utakuwa unajenga imani ya kutosha katika jamii, bali huduma yako itaaminika na kujenga heshima kwa unaowahudumia. Endelea;


1:Kama una usajili, umma kuutumikia,
Yafuate maadili, leseni yakuambia,
Janjajanja weka mbali, usije ukaumia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

2:Orodha ni kubwa kweli, wameshatutangazia,
Huduma kila mahali, watu wanahudumia,
Ni biashara halali, mwatakiwa tufanyia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

2:Malalamiko ni mengi, mikopo yatuambia,
Na hata majina mengi, jinsi watu waumia,
Watoa huduma wengi, hawazishiki sheria,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

3:Mikopo mnayotoa, watu waweze tumia,
Masharti mnatoa, ya kinyume cha sheria,
Wateja mwawakomoa, wanalia twasikia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

4:Mikataba ya mikopo, vipengele mwazuia,
Watu wapata mikopo, na kuanza ilipia,
Mwisho mwawabana hapo, wanabakia walia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

5:Kabla kukopa mtu, vema mkamuambia,
Wala msifiche kitu, kile mtamfanyia,
Achukue roho kwatu, pesa aweze tumia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

6:Huko kuwapandishia, mnakiuka sheria,
Watu wengi wanalia, jinsi mnawafanyia,
Kumbe hamkuwambia, yao kuwatimizia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

7:Aliyekopa mwenyewe, kuna muda awajia,
Mkopo wake mwenyewe, ataka jinunulia,
Azungushwazungushwa we, tamaa ajikatia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

8:Mamlaka simamizi, vema kuwafwatilia,
Malalamiko ya wazi, vema kushughulikia,
Kuondoa uonezi, na watu kulialia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

9:Kutotimiza sheria, jinsi kunavyozidia,
Kunaweza kufikia, adhabu kuwashukia,
Na mwisho mkaishia, pabaya nawaambia,
Huduma ndogo za fedha, zingatieni sheria.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news