JENGA UPEKEE WAKO-3

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA Biblia Takatifu 1 Yohana 5:20..."Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele."

Picha na Nebraskatoday.

Binti, tambua kuwa, kama bado hujajijua kuwa ni wa pekee sana, utakuwa unakosea sana, maana kujua tu wewe ni wa pekee ni silaha tosha ya kuangusha fikra nyingi potofu.

Ndiyo maana Mungu amekupa akili nyingi za kuweza kuyatambua mema na mabaya, ukitaka kuupata ukweli chukulia mfano mdogo, ukichukua mchele kwa ajili ya mapishi wakati wa kuupeta lazima utakutana na chuya katikati ya mchele, vivyo ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kila siku, tumezungukwa na wema na wabaya.

Sasa ni jukumu lako la kuhakikisha akili ambayo Mungu amekukirimia unaitumia kujitenga na wenye nia ovu na kujijengea upekee wako katika maisha. 
 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande,anasisitiza kuwa, ukitaka kuwa shujaa jenga upekee wako katikati ya wengine. Endelea;

1. Ukitaka kuwa mzuri, jichanganye na wabaya,
Ukitaka kuwa sukari, kati kuwe ladha mbaya,
Kufika hapo safari, ni kwenda pasipo haya,
Jenga upekee wako, katikati ya wengine.

2. Uwe mrembo mweusi, jangamana bila haya,
Na wabadili weusi, wawe ulayaulaya,
Nywele za kwenye utosi, utokelezee mwaya,
Jenga upekee wako, katikati ya wengine.

3. Wewe mweusi mweusi, urembo wako ni faya,
Hebu sababisha kesi, kwa mazuri si mabaya,
Siige wenye mkosi, utaishia kubaya,
Jenga upekee wako, katikati ya wengine.

4. Maisha usiwe gesi, ile ya soda ni mbaya,
Jinsi yafoka kwa kasi, unaweza ukagwaya,
Na kwa hiyo hiyo kasi, inaishia vibaya,
Jenga upekee wako, katikati ya wengine.

5. Hebu tafuta nafasi, ya kuonekana mwaya,
Fanya chanya siyo hasi, tofauti na wabaya,
Tukuone kali pisi, tubaki twashika taya,
Jenga upekee wako, katikati ya wengine.

6. Kama watu wakughasi, pengine siyo wabaya,
Sifanye yenye nuksi, ukafoka kwa ubaya,
Wasikize kwa nafasi, kama mzee wa kaya,
Jenga upekee wako, katikati ya wengine.

7. Kama hao ni mkosi, kwa upole watagwaya,
Utakijenga kikosi, wakuone si mbaya,
Kwako taanza jifosi, na yao pasipo haya,
Jenga upekee wako, katikati ya wengine.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Shairi hili ni sehemu ya Mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana (0752 352 116) wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo ameyatoa katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya Mabinti. Mashairi yatakujia katika sehemu saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news