NA FRESHA KINASA
SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia katika Mkoa wa Mara limepongezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Fadhili Maganya kwa juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women, Rhobi Samwelly akimkabidhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho (CC), Fadhili Maganya tuzo ya heshima alipotembelea Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama.
Mwenyekiti huyo, ametoa pongezi hizo jana alipotembelea Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kinachomilikiwa na shirika hilo kilichopo Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara.

Shirika la hilo, linamiliki vituo viwili ambavyo hutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni ambapo ni pamoja na Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama ambacho kipo Mugumu wilayani Serengeti na Kituo cha Nyumba Salama ambapo kipo Kiabakari Wilayani Butiama.

Rhobi Samwelly ambaye ni Mkurugenzi wa shirika hilo (HGWT), amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwaruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito wakiwa masomoni kuendelea na masomo yao jambo ambalo linawezesha kupata haki ya elimu na kufikia ndoto zao.
Pia, Rhobi amekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kutoa msisitizo kwa umma kuachana na vitendo hivyo ambavyo vinakiuka haki za binadamu na Sheria za nchi.
Aidha, Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania Rhobi Samwelly alimkabidhi tuzo ya heshima Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi na Mjumbe wa Kamati kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi, Fadhili Maganya.
Tags
Chama Cha Mapinduzi
Habari
Hope for Girls and Women in Tanzania
Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT)
Jumuiya ya Wazazi