NA VERONICA SIMBA-REA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Iringa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipowasili mkoani Iringa Machi 14, 2023 kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo, Machi 14, 2023 baada ya ziara ya Kamati hiyo kukagua Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Makamu Mwenyekiti, Japhet Hasunga alisema kuwa wamejionea kwa macho na kujiridhisha kuwa maendeleo ya utekelezaji wake ni mazuri.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipowasili mkoani Iringa Machi 14, 2023 kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) wakiwapokea Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wakati Kamati hiyo ilipowasili mkoani Iringa, Machi 14, 2023 kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
“Tumetembelea maeneo haya kukagua na kujiridhisha ikiwa yale tuliyoambiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika taarifa yao kwa Kamati ni ya kweli au la. Tunashukuru tumejionea kwa macho na kuthibitisha kuwa kweli Mradi unatekelezwa na uko katika hatua nzuri. Tunawapongeza sana REA,” alisema Makamu Mwenyekiti.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi wote waliofikiwa na umeme katika maeneo yao kuunganisha na kuutumia umeme huo majumbani na katika shughuli za maendeleo ili kujiinua kiuchumi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene (aliyesimama) akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Kamati hiyo ilikuwa katika ziara ya kazi mkoani Iringa, Machi 14, 2023 kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
Alisema kuwa pamoja na jitihada za Serikali kupeleka umeme vijijini, mojawapo ya changamoto kubwa ni kwa wananchi katika baadhi ya maeneo kutokuunganisha na kutumia nishati hiyo ilhali ipo tayari katika maeneo yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene (aliyesimama) akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Kamati hiyo ilikuwa katika ziara ya kazi mkoani Iringa, Machi 14, 2023 kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
“Nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi ambao wamefikiwa na umeme katika maeneo yao, kuunganisha na kuutumia kwa shughuli za kujiletea maendeleo kwani ndiyo lengo la Serikali. Ifahamike kwamba Serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi hii hivyo kutokuutumia umeme wakati upo ni kuitia hasara Serikali na kurudisha nyuma jitihada za kuwaletea wananchi wake maendeleo,” alisisitiza Mwenyekiti.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (aliyesimama), akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Kamati hiyo ilikuwa katika ziara ya kazi mkoani Iringa, Machi 14, 2023 kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
Awali, akiwasilisha kwa Kamati hiyo, taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Iringa, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alisema kuwa kati ya vijiji 39 ambavyo vilikuwa havijafikiwa na umeme mkoani humo, tayari vijiji 17 vimekwishafikiwa na vilivyobaki vitakuwa vimepelekewa umeme kabla ya Juni mwaka huu wa 2023 kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu alieleza kuwa, Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili mkoani Iringa unatekelezwa na Mkandarasi M/s OK Electrical & Electronics Services Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 15.6.
Kuhusu miradi mingine inayotekelezwa na REA mkoani humo, Mhandisi Saidy alisema kuwa ni pamoja na Mradi wa kusambaza umeme katika vituo vya afya na visima vya maji ili kupambana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo UVIKO – 19 pamoja na Mradi wa kusambaza umeme katika migodi midogo ya madini na maeneo ya kilimo.
Pia, alisema kuna Mradi mpya wa Ujazilizi Fungu la Pili C ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani Wakala upo katika hatua za mwisho za manunuzi kupata Mkandarasi atakayetekeleza mradi huo.
Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ni Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) pamoja na Menejimenti ya REA.