SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-5

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...lakini kwa siku hiyo aliamua kutembea kwa miguu akiwa kwenye uhalisia wake. Mfukoni alikuwa amewabeba wale wachawi wanane, alipotokeza kwenye uanda aliwaona kundi la wachawi wakiwa wamesimama na Padri yule mzungu.

Endelea

Tayari ilikuwa imetimia saa nane na dakika kadhaa, wale wachawi waliokuwa wakimsubiri walikuwa zaidi ya thelathini.

Wote hawakuwa wenyeji wa maeneo hayo, maana kama wangekuwa ni wenyeji ingemuwia rahisi mtoto huyo kuwatambua.

Kumbuka tokea siku ya kwanza ya kuzaliwa kwa mtoto huyo aliingizwa kwenye shughuli za kichawi. Kwa namna hiyo ingekuwa rahisi kwake kuwatambua wachawi hao.

Baada ya Padri yule kushindwa pale shuleni kumdhibiti mtoto huyo, aliutumia muda huo kwenda kukusanya wachawi hao ili wapambane na mtoto huyo. Lengo jingine la wachawi ilikuwa ni kuwaokoa wachawi wenzake pamoja na kumteketeza mtoto.

Mtoto yule aliendelea kutembea kwa kujiamini akielekea nyumbani kupitia maeneo waliyokuwa wamesimama wale wachawi.

Wakati huo wale wachawi mfukoni walikuwa wakilia sana, katika umri huo kijana huyo hakuwa na huruma hata kidogo.

Alipowakaribia wale wachawi kama hatua mia moja, alitumiwa nyuki na wale wachawi. Kwake yeye hilo lilikuwa ni jambo dogo, mtoto huyo alitoa mkono wa kushoto akaunyanyua juu wale nyuki wakapukutika mithili ya majani ya miti kipindi cha kiangazi.

Alipotembea hatua mbili mbele wale wachawi walituma tena mwewe wa ajabu. Mwewe huyo alikuwa na mabawa ya kawaida ila kichwa chake kilikuwa cha binadamu.

Miguu yake ilikuwa mikubwa na yenye nguvu zaidi ya miguu ya tai. Mkia wake ulikuwa mrefu mithili ya tausi wa Dodoma.

Ndege huyo alikuja akipaa kwa kasi ya kipanga, mtoto THE BOMBOM alitikisa kichwa chake huku akiendelea kutembea bila uoga.

Yule mwewe alishusha kucha zake akiwa na Lengo la kumnyakua mtoto huyo lakini tukio la ajabu lilitokea. Alitokea ndege mwingine mkubwa zaidi yake, ndege huyo wa pili alimnyakua yule ndege wa wachawi na kupaa naye hewani.

Matukio mawili yalitokea kwa muda mfupi, hata hivyo matukio hayo hayakumdhuru hata kidogo mtoto huyo. Alionekana kuwa na nguvu za ajabu kuliko umri wake, alikuwa hajafanya jambo lolote baya dhidi yao.

Mbali ya wao kumshambulia hakuwa amewalipiza jambo la ajabu, alizidi kuwasogelea maeneo waliyokuwa wamesimama wachawi hao maana njia ya kuelekea kwao ilipita eneo hilo.

Alipowakaribia zaidi kama hatua hamsini, walianza kumzunguka ili kimuweka katikati. Lengo lao lilikuwa ni kumtia mikononi mwao, kulingana na nguvu alizokuwa nazo aliyeyuka mithili ya mshumaa.

Hatimaye alipotelea ardhini mfano wa maji yaliyomwagika kwenye udongo tifutifu, wale wachawi walipoona hivyo walikimbilia eneo hilo.

Tayari walikuwa wameshagundua nia ya mtoto huyo ya kuwatoroka, hesabu zao hazikwenda vyema kwani mtoto huyo alipotelea ardhini.

Walipofika eneo hilo walijaribu kuchota mchanga wa eneo alilozama mtoto huyo. Kila walipojaribu kuuchota mchanga huo ulipotelea mikononi mwao kwa namna ya ajabu ajabu.

Uliyeyuka mfano wa barafu mbele ya joto kali, wakashauriana kumwaga dawa zaidi eneo hilo. Dawa zao hazikusaidia kitu, mtoto THE BOMBOM alikuwa ameshaondoka katika upeo wa macho yao.

Hawakuwa wakifahamu walikuwa wakipambana na mtu wa namna gani, wao walijua yule alikuwa ni mtoto wa ajabu tu mwenye nguvu za ziada za kichawi.

Hawakujua kuwa walikuwa wakipambana na kiongozi mkuu wa wachawi aliyekuwa akisubiriwa na makundi mbalimbalj ya kichawi duniani.

Baada ya mtoto THE BOMBOM kuwatoroka wachawi hao, alikwenda moja kwa moja nyumbani kwao. Alimkuta bibi yake akiwa kagubikwa na wasiwasi moyoni mwake, kitendo cha bibi huyo kuona mjukuu wake kachelewa kurudi nyumbani kilimtia wasiwasi.

Baada ya kumuona tabasamu lake lilichanua mithili ya mti wa mtende wakati wa upepo. Alimshika mkono mjukuu wake wakaingia ndani, bibi alikuwa ameshagundua jambo fulani kwa mjukuu wake.

Walipoingia ndani mtoto THE BOMBOM alijishika mfukoni kisha akawatowa wale wachawi wanane. Alimkabidhi wachawi hao kisha akaanza kumsimulia kilichojili mwanzo mwisho, wakati huo walikuwa wamesinzia huku wakiwa hawajitambui hata kidogo.

Alimuelezea namna mazungumzo yao na yule mzungu yalivyoanza, namna mzungu yule alivyoleta kimbunga. Hakukomea hapo alisimulia jinsi alivyowakamata wachawi hao baada ya kuzuia kimbunga, namna alivyowakimbia wachawi hao pale uandani.

Habari hiyo ilimsikitisha sana bibi, hasira ilikuwa kubwa sana dhidi ya kikundi hicho cha wachawi kilichokuwa kimeingia kwenye himaya yake pasipo kutoa taarifa.

Mbaya zaidi mtoto aliyekuwa akishambuliwa ni mjukuu kipenzi chake. Bibi huyo alinyanyua mkono wake juu kisha zikadondoka dawa mikononi mwake zilizokuwa zimefungwa kwenye maganda ya mahindi.

Alichukua dawa moja akatoka nje ya nyumba kisha akainyunyiza kidogo kuzunguka nyumba hiyo. Lengo la kunyunyiza dawa hiyo ilikuwa ni kuwazuia watu wa familia hiyo kuingia ndani ya nyumba hiyo.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji iwapo katika familia yenu kuna mtu anataaluma ya uchawi, kuna mambo mengine huwa yanaendelea pale nyumbani pasipo ninyi kutambua.

Dawa ya lushingisha ambayo hutokana na kitovu cha mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza miguu, bundi mwenye jicho chongo, mti wa mjandala mweupe pamoja na popo jike aliyezaliwa peke yake toka kwa mama yake ndiyo hutumika.
Dawa hii inapomwagwa nyumbani au katika eneo lengwa husaidia kuwasahaulisha wasio wahusika kuja eneo hilo. Hawawezi kuja eneo hilo mpaka mhusika atakapomwaga dawa nyingine ya kuondoa hali hiyo.

Dawa ya aina hii ipo ya aina mbalimbali kutegemea na nguvu za wachawi husika. Kuna muda shughuli za kichawi zinaweza kufanyika mchana kweupe hasa muda wa saa kumi jioni.

Shughuli hizo zinaweza kufanyika mahali popote na watu wengine msijue kulingana na dawa hizi kuwasahaulisha kupota eneo husika.

Baada ya kumwaga dawa hiyo bibi alirudi ndani, alipoingia aliwakuta wale wachawi wakiwa bado kwenye maumbo ya karatasi.

Aliwamwagia dawa ya logendo wakarudi kwenye maumbo yao halisi, aliwapaka dawa ya nsungulolo ili kuwaondoa katika hali yao ya kutojitambua.

Walishangaa wakiwa katika mazingira mageni, hata hivyo kitendo cha kumuona yule mtoto THE BOMBOM walishituka.

Mshituko wao ulikuwa wazi kabisa, hata hivyo hawakuwa na namna ya kuondoka eneo hilo. Walikuwa chini ya himaya ya bibi, ambaye alikuwa ni mchawi mkuu Wilaya ya Magu.

Bibi alimchukua mmojawao na kumpaka dawa ya kaboja, dawa hii hutokana na mchanganyiko wa nyoka kifutu, kobe wa porini, sumu ya aina fulani ya samaki na sumu ya miti fulani. Dawa hii ikisagwa na kupakwa mtu yeyote, mwili wake huweza kuoza kwa muda mfupi sana.

Wenzake walipoliona hilo walianza kulia maana walijua kuwa baada ya mwenzao wangelifuata wao. Mambo yote haya yalitendeka mbele ya macho ya mtoto THE BOMBOM, katika umri huo alikuwa anafahamu namna ya kuandaa dawa hizo na matumizi yake.

Yule mchawi alioza huku akijiona maana kichwani hakuwa amepakwa dawa hiyo, baada ya dakika kadhaa aliyeyuka na kuwa unga mtupu.

Ule unga ulikusanywa na mtoto THE BOMBOM kisha ukahifashiwa kwenye chombo fulani. Ikafuata zamu ya mchawi mwingine, alishikwa na kusogezwa eneo husika. Machozi yakawa yanamtiririka mfano wa chemchemu za mto Simiyu. Bibi hakujali hilo aliendele kumvuta.

Ndugu msomaji mambo yanasonga mbele, endelea kufuatilia simulizi hii mpaka mwisho wake.

WABEJA NKOYI

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news