Kesi ya Halima Mdee, wenzake 18 kuvuliwa uanachama CHADEMA yachukua sura mpya

NA DIRAMAKINI

MAWAKILI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameondoa nia ya kuwahoji maswali ya dodoso, Mheshimiwa Halima Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko.

Ni juu ya kiapo kinzani walichowasilisha katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam katika kesi waliyofungua kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Wabunge wengine katika shauri hilo ni Halima Mdee, Grace Tendega, Nursat Hanje, Cecilia Pareso, Hawa Mwaifunga, Esther Matiko, Esther Bulaya na Jesca Kishoa.

Pia kuna Mheshimiwa Felister Njau, Agnesta Lambart, Asia Mohamed, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Styella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza na Naghenjwa Kaboyoka.

Hatua hiyo imefikiwa Machi 6, 2023 mbele ya Jaji Cyprian Mkeha baada ya wakili wa CHADEMA, Hekima Mwasipo kuieleza Mahakama hiyo kuwa wameamua kufunga maswali hayo baada ya kutafakari kwa kina na kubaini kwamba hawana maswali ya ziada kwa wabunge hao.

Shauri hilo namba 36/2022 liliitwa mahakamani hapo kwa ajali ya Mbunge Jesca Kishoa kumalizia kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa CHADEMA kuhusu malalamiko yake ya kufukuzwa uanachama kinyume cha sheria, lakini Wakili Mwasipo akadai kuwa wamefunga kumuuliza maswali hayo.

Aidha, baada ya kuwasilisha ombi hilo, Jaji Mkeha alikubali ombi la kufunga maswali ya dodoso, kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 9,mwaka huu ambapo wajumbe watakaoanza kuhojiwa ni Dkt.Lwaitama na Ruth Molel baada ya Mdee na wenzake kutaka wajumbe hao wa Bodi ya Baraza la Wadhamini CHADEMA nao wahojiwe.

Mei, mwaka jana Kamati Kuu ya CHADEMA ilipiga kura na kuwafukuza wanachama 19 wanawake waliokuwa wanashutumiwa kwa utovu wa nidhamu kwa kosa la kuapishwa kuwa wabunge bila ruhusa ya chama chao.

Kikao hicho ambacho kilichukua muda mrefu baada ya mkutano wa Baraza Kuu uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam kiliisha kwa kura za matokeo ya jumla ya idadi ya wajumbe 423.

Aidha, waliokubalina na maamuzi ya kamati ya kuwafukuza uanachama ni 413 sawa na asilimia 97.6, wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu walikuwa ni watano sawa na asilimia 1.2 na wasiofungamana na upande wowote walikuwa ni watano sawa na asilimia 1.2.

Wanawake wa CHADEMA kupitia Baraza la Wanawake (BAWACHA) waliofukuzwa walikuwa ni makada waliokuwa mstari wa mbele kukipigania chama hicho na baada ya Baraza Kuu kubariki uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA walifukuza ndani ya chama kwa kukubali kwenda kuapishwa na kuwa wabunge kinyume cha matakwa ya chama hicho.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema siku hiyo alisema, hakuna nafasi nyingine kwa waliokuwa makada 19 wa chama hicho ya kukata rufaa.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alipoulizwa baada ya kutoka hapo alisema hawakuwa na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kufuata katiba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news