NA MWANDISHI WETU
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Mhe. Stanslaus Mabula (Mb) imekagua ujenzi wa madarasa saba na matundu ya vyoo 22 katika Shule ya Sekondari Lwiche katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Ujenzi wa madarasa saba na matundu ya vyoo 22 yamejengwa kupitia fedha za mapato ya ndani pamoja na michango kutoka kwa wadau na wananchi ikiwa ni pamoja na mfuko wa jimbo kwa jumla ya shilingi milioni 154.
Wakati akisoma taarifa Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Lwiche, Mwalimu Sophia Yamsebo amesema kuwa, wananchi walishiriki katika kutoa nguvu kazi ikiwa ni pamoja na kukusanya mawe, mchanga na kusomba pamoja na kufanya kazi za kuchota maji, kusogeza tofari na kuchimba mashimo ya vyoo.
Mwalimu Sophia Yamsebo ameeleza kuwa, kiasi cha shilingi milioni 116.8 kimetokana na mapato ya ndani ya halmashauri na kiasi cha shilingi milioni 37.5 kimetokana na nguvu za wananchi na mfuko wa jimbo.